Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume wanapoundiwa mkakati ili wapime VVU

9458 Pic+wanaume TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sasa kuna tumaini jipya baada ya kupatikana kwa dawa ya kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi ambayo wagonjwa watatakiwa waanze kuitumia mapema tofauti na awali.

Dawa hiyo ina uwezo wa kupunguza makali ya virusi kwa kiwango kikubwa na kumpunguzia mwathirika uwezekano wa kuambukiza wengine.

Pia dawa hiyo humfanya mgonjwa kuishi maisha marefu na ya furaha tofauti na ilivyokuwa awali wakati mgonjwa alikuwa anaonekana kama tishio kwa jamii.

Mkakati mpya wa Serikali wa kupima na kumuanzishia dawa mapema mtu anayegundulika kuwa na virusi bila kujali kiwango cha CD4, unakuja wakati kuna idadi ndogo ya wanaume wanaotambua hali za afya zao ikilinganishwa na wanawake.

INAENDELEA UK 28

INATOKA UK 27

Wakati kampeni ya upimaji VVU na kuanza dawa inayowalenga wanaume ilizinduliwa Dodoma Juni 19 mwaka huu, ni asilimia 45 pekee ya wanaume wanaoishi na VVU ambao ndio wanaotambua kuwa wana maambukizi kwa mujibu wa utafiti wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Kampeni hiyo ya kitaifa inayofahamika kwa jina la “Furaha Yangu” yenye kaulimbiu ya “Mwananume Jali Afya Yako, Pima VVU” ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikilenga kushawishi wanaume kutumia huduma hiyo kutokana na wengi wao kuhofia kupima.

Tacaids na malengo

Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Laonald Maboko anasema moja ya majukumu ya taasisi hiyo ni kuratibu tafiti kubwa za viashiria vya Ukimwi kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) pamoja na wadau wengine.

Anasema takwimu za utafiti uliofanywa na NBS zinaonyesha kuwa ni asilimia 52 tu ya wanaoishi na VVU wanatambua kuwa wana maambukizi ambao kati yao wanaume ni asilimia 45 na wanawake ni asilimia 56.

Anasema kampeni hiyo ni matokeo ya utafiti wa awali wa nne uliofanywa na NBS, ambao unaonyesha pamoja na mambo mengine, hamasa miongoni mwa wananchi na hasa wanaume katika kutumia huduma za upimaji wa VVU nchini ni ndogo.

Dk Maboko anasema lengo ni kufikia asilimia 90 ya wanaoishi na VVU ili kuwawezesha kujua wana maambukizi ifikapo mwaka 2020.

Alisema baada ya uzinduzi mikoa yote itahimizwa kufanya kampeni kubwa za mapambano dhidi ya Ukimwi kwa miezi sita, ikitakiwa kushirikiana na wadau.

Anasema Tacaids kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-Tamisemi na Wizara ya Afya kwa kutumia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) watafuatilia na kutathmini maendeleo ya mapambano na kutoa taarifa katika maadhimisho Siku ya Ukimwi Desemba mosi, 2018.

“Lakini (Shirika la Misaada la Marekani) USAID kwa kutumia mradi wa Tulonge Afya chini ya FHI360, wataendeleza ufadhili wa kampeni hizi kwa miaka mitano, hususan katika mikoa iliyo katika mradi husika,” anasema.

Dk Maboko anasema katika kampeni hiyo wanatarajia kuwa na matokeo chanya kama kuongezeka kwa idadi ya wananchi waliopima na kufahamu hali zao, hasa wanaume na kuongezeka kwa idadi ya wanaotumia dawa za kufubaza VVU.

Serikali na mkakati wa upimaji

Kaimu mkurugenzi kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk Angela Ramadhani anasema kampeni hiyo inahamasisha mkakati mpya wa Serikali wa upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV mapema kwa wale watakaokutwa na VVU.

“Katika dira ya kuwa na taifa bila Ukimwi, Tanzania imeridhia malengo ya UNAIDS ya 90-90-90, yaani asilimia 90 ya watu wote wanaoishi na VVU kutambua hali zao za VVU, asilimia 90 ya wenye maambukizi kuanza dawa na asilimia 90 ya walioanza dawa kupunguza kiwango cha VVU mwilini,” anasema Dk Angela.

Anasema kampeni hiyo iliyozinduliwa Dodoma, ilikuwa na siku tano za kutoa huduma za afya bila malipo kuanzia Juni 18.

“Wakati huu tukizungumzia kampeni ya ‘Pima na Tibu’ tunaheshimu kazi mbalimbali zilizochangia kushuka kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi VVU kutoka asilimia 7 mwaka 2003 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/17.

“Licha ya mafanikio haya, tumedhamiria kuendeleza mapambano hadi tutakapotokomeza janga hili nchini Tanzania. Hii ndiyo sababu leo tunashirikiana kutangaza kampeni mpya ya ‘Kupima VVU na Kuanza ARV Mapema’.”

Dk Angela anasema dhamira ya Serikali ya Tanznaia ni katika kuhakikisha huduma za VVU na Ukimwi zinapatikana chini ya kampeni ya kupima na kuanza dawa mapema na kuunga mkono juhudi za kuhakikisha kila mmoja anafahamu huduma hizo na kuzitumia.

Anasema wizara inatambua umuhimu wa huduma bora na uwezo wa watoa huduma, ndiyo maana inatumia wahudumu waliopitia mafunzo ya VVU na Ukimwi.

“Lakini pia tunaendesha mafunzo ya kuwaandaa watoa huduma ili kutoa huduma bora wakati wa kampeni hii ya mkakati wa kupima na kuanza dawa mapema,” amesema.

Kaimu mkurugenzi wa USAID, Ananthy Thambinayagam ameipongeza Serikali kwa uongozi na ushiriki wake katika kuendeleza kampeni hiyo.

“USAID inajivunia kuwa mdau wa muda mrefu wa kazi hii ili kutokomeza janga la VVU nchini Tanzania na duniani kote,” anasema.

“Na tumedhamiria kuendelea na ushirika wetu na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha juhudi zetu.”

Anasema kampeni hiyo kupitia mradi wa USAID Tulonge Afya umepewa mamlaka ya kuchochea fursa kwa Watanzania kuboresha hali zao za kiafya kwa kubadili mila na desturi potofu ili kuishi katika misingi bora ya kiafya kwa kutumia njia za mawasiliano ya kubadilisha tabia kwenye jamii.

Thambinayagam anasema mpango huo unalenga katika kukabiliana na maeneo ya kipaumbele ya afya, kama kukabiliana na Ukimwi, kifua kikuu, malaria na kuhamasisha uzazi wa mpango na afya ya uzazi na afya ya mama na mtoto.

“Mradi huu unawakilisha mchango muhimu wa kuiwezesha Tanzania (kuwa taifa) lenye afya bora,” anasema

Kampeni hiyo inasimamiwa na Wizara ya Afya kwa kutumia mpango wa NACP. Inashirikiana na Tacaids na USAID

Chanzo: mwananchi.co.tz