Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume waathirika zaidi saratani ya koo

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tafiti zinaonyesha wanaume wana uwezekano wa kupata saratani ya koo mara tatu zaidi ya wanawake.

Ikumbukwe kuwa, aina hii ya saratani licha ya kuwa wapo wanaotibiwa na kupona, lakini karibu aina zote za tiba huwa na madhara kwa mgonjwa na wakati mwingine kusababisha kifo badala ya kuponya.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema saratani hiyo inakuja kwa kasi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Mwaka 2018, saratani ya koo imejitokeza sana na kuwa ya tatu kati ya saratani kubwa tano kwa kuathiri Watanzania wengi kwa miaka ya nyuma ilikuwa nafasi ya nne,” anasema Waziri Ummy.

Mkurugenzi Kitengo cha Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Dk Crispin Kahesa anasema ingawa bado hakuna visababishi kamili vya saratani hiyo, sababu hizo hujitokeza kwa walio wengi.

Alisema asilimia 90 ya wagonjwa wa saratani ya koo wamekuwa na historia ya uvutaji sigara, unywaji pombe kali kama viroba na kula aina za vyakula vilivyochomwa ikiwamo nyama na samaki, ulaji pilipili, ndimu, ‘chilisosi’ na unywaji wa vitu vya moto kupita kiasi.

“Ongezeko ni kubwa, asilimia 90 ya wagonjwa tuliowapokea hapa wana historia ya kutumia vilevi vikali, sigara, pilipili kwa wingi na aina nyingine na vitu vinavyosababisha saratani hii,” alisema Dk Kahesa.

Alisema kuwa saratani ya koo ni mbaya zaidi ukilinganisha na saratani za aina nyingine.

Alisisitiza, “Kwa bahati mbaya ni asilimia tano pekee ya wanaopata saratani hii wanapona. Ukimwona mgonjwa unaweza kulia, hawezi tena kula na ikibidi huingiziwa mipira maalumu ili kupitisha chakula, lakini kuna wakati hata mipira huziba, hivyo huishi kwa dripu ya chakula pekee.”

Dk Kahesa ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani, alisema mwaka 2017 saratani ya koo ilishika namba nne kati ya saratani zinazosumbua hapa nchini lakini mwaka 2018 imeshika nafasi ya tatu.

Alisema kunakuwa na mabadiliko kadri muda unavyokwenda kwani siku za nyuma asilimia 66 ya saratani zilisababishwa na virusi.

“Mwaka 2015 kulikuwa na wagonjwa wapya wa saratani hii 643, mwaka 2016 wakafikia idadi ya 657 na 2017 waliogundulika ni 699 unaona hapo ilikua kwa kasi.”

Mgonjwa aliyelazwa kwenye taasisi hiyo akitibiwa saratani ya koo, Baltazari Tarimo (51) alisema kuwa aliugua maradhi hayo mwaka jana ambapo anaamini yametokana na mfumo wake wa maisha.

“Nilikuwa mnywaji mzuri tu, bia konyagi nilikuwa nakunywa na sigara niliweza kuvuta mpaka kipindi naanza kuugua maradhi haya nilikuwa bado navuta, awali nilipougua nilitibiwa kwa muda mrefu na tiba asili ila nashukuru baada ya matibabu hospitalini ninaendelea vizuri,” alisema Tarimo.

Dalili zake

Dk Kahesa anasema aina zote mbili huanza kwa kuathiri seli zilizo katika utando wa ndani wa ukuta wa koo, uitwao ‘mucosa’ kabla ya kusambaa maeneo mengine.

Na katika hatua za awali, mgonjwa mwenye saratani ya koo anaweza asionyeshe dalili zozote. Hata hivyo, kadri saratani inavyozidi kukua na kuenea, mgonjwa anaweza kuanza kuona dalili.

“Dalili ya kwanza ya mgonjwa wa saratani ni chakula kukwama kwenye koo, siku za mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa kumeza chakula kigumu kisha cha majimaji na baadaye akashindwa kumeza hata mate.

“Maumivu wakati wa kumeza chakula, hasa chakula kigumu, maumivu kwenye kifua au mgongoni, kupungua uzito, kiungulia na sauti ya mkwaruzo au kikohozi kikavu cha zaidi ya wiki mbili,” alisema.

Hata hivyo, alisema wapo wanaopata saratani kwa kurithi kutoka kwa wazazi wao pamoja na umri kuwa mkubwa pia huchangia tatizo hilo.

Utafiti

Kwa mara ya kwanza mwaka 1983 hadi 1992, Taasisi ya Afya ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ilifanya utafiti na kubaini kuwa kati ya wagonjwa 546 waliopimwa kulikuwa na wastani wa wagonjwa 116 wanawake huku 430 wakiwa ni wanaume.

Utafiti huo ulifanywa na Dk Henry Mwakyoma kwa kushirikiana na Dk N Mbebati, Dk M Aboud, Dk J Kahamba na Dk C Yongolo uliokamilika Juni 1, 1994, ambao ulibaini ukuaji wa saratani ya koo Kanda ya Kaskazini kwa watu wa umri kati ya miaka 50-59.

Watu wenye umri kuanzia miaka 21 hadi 90 walishiriki na wagonjwa wengi walikuwa wenye umri wa miaka 50-59 hali ambayo ni tofauti na sasa ambapo ni kuanzia miaka 30 hadi 50.



Chanzo: mwananchi.co.tz