BAADHI ya wanaume tumekuwa na mtazamo kuwa ugonjwa wa saratani ya matiti, unawapata wanawake tu na hivyo hata upimaji wa saratani hiyo, unawahusu wao zaidi.
Lakini ukweli ni kwamba hata wanaume tunaweza kupata saratani hiyo, licha ya kuwa hatuna matiti, ila sehemu zetu mbili za vifua ndizo zinaweza kuchukuliwa kama matiti huku sababu za kupata ugonjwa huo kwa wanaume na wanawake zikiwa hazitofautiani sana.
Hata hivyo, idadi ya wanaume kupata saratani hiyo ni ndogo, ikilinganishwa na ile ya wanawake, ambapo katika watu 100 mwanaume mmoja anaweza kuwa na saratani hiyo, huku wanawake 99 wanaweza kuwa na ugonjwa huo.
Kukosekana kwa elimu ya kutosha ya saratani hiyo, imekuwa ni sababu kubwa ya wanaume kutopima.
Oktoba 31 ilikuwa kilele cha mwezi wa maadhimisho ya saratani ya matiti ambayo ni Oktoba ya kila mwaka. Siku hiyo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ilifanya upimaji wa saratani hiyo, ambapo wanaume zaidi ya 100 jijini Dar es Salaam walijitokeza.
Binafsi napenda kuungana na taasisi hiyo kuhamasisha wanaume wengi zaidi, kujitokeza ili kujua afya zao na kuchukua hatua mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa.
Ifahamike kuwa kama mtu akichelewa kupima, anaweza kuathirika na hata kufika hospitalini akiwa ameshafikia hatua ya tatu na nne, ambazo ni hatua za mwisho zinazosababisha mgonjwa kutopona.
Nianze kuwafahamisha kuwa mwanaume kama ilivyo kwa mwanamke, anaweza kupata ugonjwa huo kwa kurithi vinasaba kutoka katika familia yake.
Pia umri mkubwa wa kuanzia miaka 50, unaweza kusababisha saratani hiyo. Pia mtindo wa maisha, unene kupita kiasi na msongo wa mawazo.
Hivyo basi kuna haja ya kuanza kubadilisha mtindo wa maisha, kama kuepuka kuvuta sigara na kunywa pombe na kufanya mazoezi ili kuepuka kuwa na uzito uliopitiliza ili saratani isitokee.
Nashauri uzingatiwaji wa mlo kamili pamoja kula kwa wakati, kujiepusha na mionzi mikali hasa hii kwa wanaume wanaofanya kazi maeneo yenye mionzi mikali na kutumia vifaa vya kujikinga, ambavyo vitawaondoa katika hatari ya kupata ugonjwa huo.
Kama ukipata uvimbe usio na maumivu kwenye titi moja au matiti yote, uvimbe unaoongezeka kadiri siku zinavyokwenda huku ngozi ya matiti inaanza kuwa na rangi nyekundu au kidonda, hiyo ni dalili ya saratani.
Mnaweza kujipima kwa kukaa kifua wazi, huku ukijitazama kwenye kioo, nyanyua mkono juu na viganja vishikane juu ya kichwa chako, kisha chunguza kama kuna mabadiliko yoyote katika mlingano wa ukubwa wa matiti. Kama moja litaonekana kuwa kubwa zaidi ya jingine, basi ni moja ya viashiria vya athari ya saratani.
Naomba wanaume kwa pamoja, tujitokeze kupima saratani ya matiti, hamasishaneni ili kwa pamoja tuweze kuikabili saratani hiyo.