Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaume milioni 4.4 watahiriwa Tanzania

84445 Pic+wanaume Wanaume milioni 4.4 watahiriwa Tanzania

Fri, 15 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jumla ya wanaume milioni 4,456,511 wamefanyiwa tohara kinga ya kitabibu tangu 2009 ilipoanza kutolewa hadi kufikia Septemba, 2019.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Novemba, 15, 2019 na Ofisa Mpango kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk Sasan Mmbando wakati wa semina ya kuwajengea uelewa wabunge wa Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na kamati ya  Katiba na Sheria kuhusu mpango huo.

Dk Mmbando amesema kuwa lengo la kwanza la afua hiyo lilikuwa kuwafikia wanaume na vijana milioni 2.8 kufikia Septemba, 2017.

“Hadi kufikia Septemba, 2017 tuliweza kuwafikia milioni 3,303,940 na kuwatahiri,” amesema.

Aidha, amesema katika lengo la pili kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 wana mpango wa kuwafikia wanaume milioni 2.7.

Amesema hadi kufikia Septemba, 2019, tayari wameweza kuwatahiri jumla ya wanaume 1,681,070 ikiwa ni sawa na asilimia 60 ya lengo.

Amesema afua hiyo inatekelezwa katika mikoa 17 yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya HIV na kiwango kidogo cha utahiri nchini.

“Hata hivyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ili kuwa na huduma endelevu na kupunguza matatizo ya njia ya mkojo, mfano UTI, ilianza kutoa huduma ya tohara kwa watoto wachanga wenye umri kuanzia siku moja hadi 60, 2013, kama utafiti wa kujifunzia (pilot study), katika mkoa wa Iringa hadi sasa imefikia mikoa 15 nchini,” amebainisha.

Amesema hadi kufikia Septemba, 2019 jumla ya watoto wachanga 13,603 wametahiriwa.

“Tohara ya watoto wachanga inafanyika katika mikoa 15, Iringa Njombe, Morogoro, Singida, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Rukwa, Katavi, Songwe, Mbeya na Kigoma,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz