Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaougua kiharusi wazidi kuongezeka nchini

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umeonyesha idadi ya wanaougua ugonjwa wa kiharusi huenda ikaongezeka kutoka asilimia 8.4 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 11 mwaka 2018.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu Oktoba 29, 2018 mtaalamu wa magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu Muhimbili, Dk Mnacho Mohammed amesema utafiti uliofanywa mwaka 2015 ulionyesha idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika kulazwa hospitali hapo wakiugua kiharusi.

“Mwaka 2015 Muhimbili tulifanya utafiti mdogo kuangalia ni kwa kiwango gani wagonjwa wanaolazwa kwetu wanaugua ugonjwa huu, utafiti ulihusisha wodi ya Mwaisela ambayo watu 7,618 walilazwa pale na tatizo la kiharusi lilichangia asilimia 8.4 wagonjwa takribani 642 walilazwa kwa tatizo hilo,” amesema Dk Mnacho.

Amesema utafiti huo ulionyesha idadi ya wagonjwa wanaolazwa kwa mwaka na idadi inayochangiwa na kiharusi peke yake ni asilimia 8.4, hivyo kuonyesha ukubwa wa tatizo.

“Baada ya utafiti wetu, tumeendelea kufuatilia kila mwaka kunakuwa na kuongezeka kwa wagonjwa wa kiharusi kutokana na kuongezeka kwa magonjwa haya ya shinikizo la juu la damu na kisukari, mwaka 2018 tunategemea wagonjwa wa kiharusi peke yao watafikia asilimia 11, tunapokea kwa wingi wagonjwa hawa kwa sasa,” amesema.

Mganga Mkuu wa Serikali amesema kiharusi ni ugonjwa wa ghafla unaotokana na ubongo kukosa hewa na virutubishi, kwa sababu ya kuziba au kupasuka kwa mshipa ya damu inayosambaza damu kwenye ubongo, hali ambayo huchangiwa na kudhoofika kwa mishipa hiyo ya damu.

“Kuna aina tatu za kiharusi, kipo kinachosababishwa na kuziba kwa mshipa wa damu au mshipa wa damu inayopeleka damu kwenye ubongo “Ischemic stroke” na huwatokea watu pale ambapo bonge la damu au la mafuta linapoganda na kuzuia damu kufika kwenye ubongo,” amesema.

Ameitaja aina ya pili kuwa ni “Hemorrhagic stroke” ambayo hutokea wakati mshipa wa damu ulio dhaifu unapopasuka na ya tatu ni  ‘Transient ischemic attacks’ au “mini stroke ambayo hutokea pale mzunguko wa damu unaposhindwa kufika kwenye sehemu ndogo ya ubongo na baada ya muda mzunguko huendelea kama kawaida.

Chanzo: mwananchi.co.tz