Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaougua dengue waanza kupungua

59871 Pic+dengue

Mon, 27 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imesema wagonjwa wanaoripotiwa kuugua homa ya dengue wameanza kupungua, huku ikitaja idadi ya watu zaidi ya 2,900 kuugua homa hiyo tangu Januari.

Kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini, Wizara ya Afya, Catherine Sungura alisema jana kuwa wagonjwa hao wamepatikana Dar es Salaam na Tanga na mmoja kutoka Singida.

“Kulinganisha na hali ilivyokuwa wiki mbili zilizopita, ambako kwa wastani idadi ya walioripotiwa kwa wiki walikuwa 525 hivi sasa idadi ni 420 kwa wiki,” alisema.

“Kwa takwimu tulizonazo, tangu ulipotokea tena Januari, hadi sasa watu zaidi ya 2,900 wameugua ugonjwa huo na wawili wamepoteza maisha japo waliofariki walikuwa na maradhi mengine pia.”

Kwa nini mijini?

Alisema maeneo ya mijini ndio huathirika zaidi ikilinganishwa na vijijini kutokana na tabia na mazingira ya mbu anayeeneza ugonjwa huo ambao hauna tiba ya moja kwa moja wala chanjo kwa sasa.

Pia Soma

Alisema mbu hao hupenda kuishi katika maeneo yenye joto, maji safi na pia hupendelea kukaa katika mazingira safi.

Kuhusu tiba alisema hutegemea na hali ya mgonjwa, “kama ni katika hatua za mwanzo itajumuisha matumizi ya dawa za kuondoa maumivu (kama Paracetamol) na matumizi ya maji kwa wingi.

“Iwapo mgonjwa atakutwa na ugonjwa mkali zaidi, tiba itatolewa katika vituo vya kutolea huduma kuendana na hali hiyo,” alisema Sungura.

Ukweli kuhusu dengue

Ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya Aedes, mbu mweusi mwenye madoa doa meupe ya kung’aa ambaye hupendelea kuuma hasa wakati wa asubuhi, mchana na jioni.

Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa na kichwa hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati siku ya tatu hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya dengue.

Aidha, mgonjwa wa homa ya dengue mara chache hupata vipele vidogovidogo, anavilia damu kwenye ngozi na wengine kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia kwenye njia ya haja kubwa au ndogo.

“Katika mlipuko huu uliotokea nchini, wagonjwa wengi hawana dalili za kutokwa damu au kuvilia damu kwenye ngozi,” alisema Sungura.

Awali, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi alisema Serikali kwa kushirikiana na wananchi, viongozi na wadau mbalimbali wanaendelea na jitihada za kudhibiti ugonjwa huo.

Aliwataka wananchi na viongozi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira.

Kuhusu matibabu, Profesa Kambi alisema Serikali imehakikisha hospitali na vituo vyake vya afya vinakuwa na uwezo wa kupima ugonjwa huo huku vitendanishi vingine vikiendelea kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Bohari ya Dawa (MSD), kati ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara walivyopokea wiki inayoishia Mei 24, vilikuwamo vipimo vya homa ya dengue na kwamba wanategemea kupokea vipimo vingine 12,000 hivi karibuni.

Chanzo: mwananchi.co.tz