Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaougua Corona wapo hatarini kupata matatizo ya akili na moyo

60c7e639baa5a81907dcd70f922255ab Wanaougua Corona wapo hatarini kupata matatizo ya akili na moyo

Mon, 4 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATAALAMU wa afya wamesema, waliowahi kuugua Corona wapo hatarini zaidi kupata madhara zaidi hata baada ya kupona hususani matatizo ya akili .

Hayo yameezwa na Muhadhiri Mwandamizi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tafiti na Machapisho kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Bruno Sunguya katika katika mahojiano maalum kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona na changamoto mpya za afya zinazoibuka,’

Amesema waliowahi kuugua Corona wanapaswa kuchukua tahadhari zaidi za kujilinda na kuachana na imani potovu kuwa aliugua basi amejitengenezea kinga ya ugonjwa huo.

“Covid 19 ni ugonjwa hatari, mtu akishaugua anapata madhara mwilini hata kama atapumua vizuri na kuendelea na shuguli zake lakini atambue madhara yanayobaki mwilini ni makubwa, kawaida Corona inaadhiri viungo mbali mbali vya mwili, hata baada ya kupona changamoto zinaendelea ingawa utajiona upo sawa, ule ugonjwa uliondoka unaacha makovu.

“Jaribu kufikiria kwenye mapafu yako kukawa na makovu, au vidonda au mchubuko, hivyo hali ya mapafu kufanya kazi kawaida inakuwa imeondoka,” amesema Dk Sunguya na kuongeza

“Pia asilimia kubwa baada ya kupata Corona, wanapata ugonjwa wa sukari na kuna athari nyingine mpaka za kiakili katika ubongo wa mwanadamu,. kupona ni suala moja, lakini athari baada ya kupona ni suala jingine. Tafiti zinaendelea kufahamu hasa ni kwa nini hali hiyo inatokea na namna ya kudhibiti hali hiyo.” alisema na kuongeza

“Unaweza kupata Corona ukakohoa kidogo ukapona athari zinazobaki ni kubwa, ni vizuri jamii ikajilinda kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono na sabuni na maji tiririka, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, mtu ukipata fursa ya chanjo achome, Corona ni mbaya, ipo na imeshaua watu milioni nne hadi sasa duniani na wengine milioni 191 wanaugua.”alisema

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, kupitia Shirika la Afya Dunia (WHO) mpaka Septemba 28 jumla ya wagonjwa 25,846 wameripotiwa huku wagonjwa 719 wakipoteza maisha

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Profesa Mohamed Janabi, amesema uharibifu wa mwili unaosababishwa na COVID-19 ni mkubwa

Amesema ingawa COVID-19 inaonekana kama ugonjwa ambao huathiri sana mapafu, inaweza kuharibu viungo vingine vingi pia. Uharibifu wa ugonwa huo unaweza kuongeza hatari ya shida za kiafya za muda mrefu. Viungo ambavyo vinaweza kuathiriwa na COVID-19 ni pamoja na ;-

Moyo: Uchunguzi uliofanywa miezi kadhaa mtu baada ya kupona ugonjwa wa Corona inaonyesha anapata uharibifu wa kudumu kwa misuli ya moyo, hata kwa watu ambao walipata dalili laini tu za COVID-19.

Hii inaweza kuongeza hatari ya kushindwa kwa moyo au shida zingine za moyo katika siku zijazo.

Mapafu: Aina ya homa ya mapafu mara nyingi inayohusishwa na COVID-19 inaweza kusababisha uharibifu wa muda mrefu kwa mifumo midogo ya hewa kwenye mapafu.

Tishu inayosababishwa na kovu inaweza kusababisha shida za kupumua kwa muda mrefu.

Ubongo: Hata kwa vijana, COVID-19 inaweza kusababisha kifafa na kiharusi hali inayosababisha kupooza kwa muda.

COVID-19 pia inaweza kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kutetemeka na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Mwanafunzi wa masuala ya Saikolojia Gabriel Msumba, amesema hofu, mawazo, wasiwasi, taharuki, kuyumba kwa kipato vyote hivyo vinavyomkabili binadamu vinaweza msababishia afya ya akili.

Aidha amesema ukosefu wa ajira, hofu ya maisha pia yanasababisha msongo wa mawazo.

Amesema nchi ambazo wananchi wamewekwa Karantini baadhi yao wamepata matatizo ya akili kutokana na msongo wa mawazo. Hiyo imesababishwa na kushindwa kuishi maisha ya kawaida waliyozoea

Tiba:

Msumba amesema tiba ya matatizo ya akili inategemea jamii kwa jamii.

“Kuwatambua wagonjwa wa magonjwa ya akili ni wao kukubali wana hilo tatizo ili kuwasaidia kuwaweka kwenye uwangalizi ambao utawasaidia kuwarudisha kwenye hali ya kawaida ya ubinadamu,”alisema

Chanzo: www.habarileo.co.tz