Wanasayansi nchini Marekani wametoa matokeo ya utafiti mpya unaohusisha matumizi ya baadhi ya bidhaa za kunyoosha nywele 'hair relaxer' na ongezeko la saratani kwa wanawake.
Matokeo ya tafiti za awali yalibainisha kuwa kemikali za kunyoosha nywele zinahushishwa na hatari ya kuongezeka kwa saratani zinazohusiana na homoni, saratani ya matiti na Ovari kwa wanawake, lakini matokeo ya utafiti mpya yanaonyesha ongezeko kubwa la saratani ya Uterasi kwa wanawake kutokana na matumizi makubwa ya bidhaa hizo.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya huko Maryland, Marekani, kati ya wanawake ambao hawakutumia bidhaa za kemikali kunyoosha nywele katika kipindi cha miezi 12 iliyopita asilimia 1.6 walipata saratani ya Uterasi katika umri wa miaka 70 lakini karibu asilimia nne ya wanawake ambao hutumia mara kwa mara bidhaa kama hizo walipata saratani ya Uterasi walipofikisha umri wa miaka 70.
Utafiti huo pia umebainisha kuwa ni nadra kwa idadi kubwa ya wanawake kupata saratani ya Uterasi, hivyo ongezeko hilo kubwa linaibua wasiswasi mkubwa.
Wanasayansi waliofanya utafiti huo wamesema kuwa, wanawake wanaotumia bidhaa hizo za kunyoosha nywele mara kwa mara ndani ya kipindi cha mwaka mmoja (zaidi ya mara nne), wapo katika hatari mara mbili zaidi ya kupata saratani hiyo.