Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaotapisha vyoo wawekewa mkakati

5e0eedd36060c17fa257d27ff817ef7a Wanaotapisha vyoo wawekewa mkakati

Thu, 12 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na maofisa mazingira wa majiji, manispaa na halmashauri zote nchini, wamejipanga kudhibiti wakazi wenye tabia ya kutapisha vyoo hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka alisema hawatakuwa na huruma wala kurudishwa nyuma na watu ambao wamekuwa kikwazo katika kulinda na kutunza mazingira.

“Hivi karibuni mtakumbuka kuwa nchi yetu imeingia katika uchumi wa kati na hiyo imetokana na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika nyanja ya uchumi, afya, mazingira na sekta nyingine. Hatutaki kurudi tena katika zama za kipindupindu hasa katika Jiji la Dar es Salaam,” alisema.

Katika kuhakikisha wanadhibiti hali ya utapishaji, alisema NEMC imejipanga kushirikiana na maofisa mazingira wa majiji, manispaa na halmashauri kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wote.

“Baraza linashirikiana kwa ukaribu na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa) kuhakikisha maofisa mazingira wa jiji, manispaa na halmashauri zote nchini wanasimamia sheria, taratibu na kanuni za mazingira ikiwemo suala la utapishaji kwenye maeneo ya makazi ya watu,” alisema.

Dk Gwamaka aliwaomba Watanzania kuendelea kushirikiana na NEMC hususani kupitia kitengo chake cha timu ya dharura ambacho kinafanya kazi kwa saa 24 kila siku kwani mafanikio makubwa yameshapatikana.

“Wito wangu kwa Watanzania wasichoke kutoa ushirikiano kwa baraza hasa kwa kitengo chetu cha dharura ambacho kimekuwa kikifanya kazi nzuri kwa saa 24 ili kukabiliana na changamoto za mazingira kwa kuwa watumishi wa chombo hicho hawawezi kuwa kila mahali,” alisema.

Alisema utapishaji majitaka na utapishaji wa vyoo huhatarisha jamii kiafya na ni kosa hivyo, yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

“Kuna taarifa tunazipata kutoka kwa watu mbalimbali kuwa changamoto hii ya kutapisha vyoo inatokana na hasa gharama zinazodaiwa kuwa kubwa za ukodishaji magari ya taka ambayo yamekuwa yakinyonya majitaka katika makazi ya watu. Nawashauri kuunganisha nguvu ya watu wawili au watatu ili waweze kupata gari ambayo itanyonya majitaka kuliko kuyatiririsha kwenye makazi ya watu kinyume na sheria ya mazingira,’’ alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz