Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaojitolea sekta ya afya kupewa kipaumbele ajira

829f50cf7ba4de9453b2ea51349327e5 Wanaojitolea sekta ya afya kupewa kipaumbele ajira

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema itatoa kipaumbeke cha ajira kwa watumishi wanaojitolea katika hospitali za serikali.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali ya Uhuru iliyopo wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Alisema hatua hiyo ni kuonesha serikali inatambua na kuthamini mchango wa watumishi wanaojitolea katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Niwatoe hofu watumishi wanaofanya kazi za kujitolea katika hospitali kuwa serikali itawapa kipaumbele katika ajira zitakazotolewa,” alisema.

Ummy aliwaagiza waganga wakuu wa wilaya kote nchini kuhakikisha wanakuwa na kanzidata ya watumishi wanaojitolea katika vituo vya kutolea huduma za afya.

"Naagiza waganga wakuu wa wilaya mkasimamie hili na kwenye kanzidata watumishi hao waainishwe wameanza kujitolea lini, isije kuwa kesho wakafurika watu wa kujitolea baada ya kusikia watapewa kipaumbele kwenye ajira," alisema.

Kuhusu Hospitali ya Uhuru, Ummy aliagiza kuanza ujenzi wa majengo ya awamu ya pili ili kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya.

“Baadhi ya huduma kuanza kutolewa katika hospitali hii, ni vyema kuanza mchakato wa ujenzi wa majengo ya awamu ya pili yatakayojumuisha wodi za kulaza wagonjwa.”

“Hapa tumeona kazi kubwa imefanyika, zimebaki kazi ndogo ndogo ili ujenzi wa awamu ya kwanza ukamilike, naona na huduma zinatolewa, sasa tuanze mchakato wa ujenzi wa awamu ya pili tujenge wodi, hapa ni barabarani lazima tupanue zaidi huduma," alisema.

Waziri huyo alisema serikali itatoa Sh bilioni 1.7 zinazohitajika ili kukamilisha kazi ndogo ndogo zilizobaki ili kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi.

"Tuwahamasishe wananchi wajiunge na Mfuko wa Bima ya Afya, ukiangalia kuna wagonjwa kujiandikisha tu anatoa Sh 15,000 wakati angekuwa na bima hata ya Sh 30,000 asingelipa hiyo 15,000," alisema.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Athumani Masasi alisema ujenzi ulianza rasmi Novemba 26, mwaka 2019 kwa kutumia akaunti maalum ‘force account’ kwa kumtumia mkandarasi Suma-JKT na mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 98.2.

Alisema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje tangu Desemba 21, mwaka jana, inawatumishi 52 kati ya 117 wanaohitajika na mpaka sasa imehudumia wagonjwa 3,154 na imekusanya zaidi ya Sh milioni 33.

Hospitali ya Uhuru imejengwa baada ya aliyekuwa Rais wa wa Awamu ya Tano, John Magufuli kuahirisha maadhimisho ya Siku ya Uhuru ya Desemba 9 mwaka 2018 na kuelekeza fedha zilizokuwa zitumike kufanikisha maadhimisho hayo kufanya ujenzi huo.

Ummy pia alifanya ziara katika shule ya watu wenye mahitaji maalumu ya Buigiri inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika kwa kushirikiana na serikali na ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo.

Mkuu wa shule hiyo, Samuel Jonathani alisema ina wanafunzi 118 wenye ulemavu wa aina mbalimbali na wamekuwa na ufaulu wa asilimia 98 hadi 100 kwa miaka 10 mfululizo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz