Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaochukua 50,000/- afya kwa watoto kukiona

442ad602cf6f340d35f6784575e8d59b Wanaochukua 50,000/- afya kwa watoto kukiona

Mon, 30 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI wilayani Mbarali mkoani Mbeya imeahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya akinamama wanaojifungulia majumbani kutozwa rushwa ya hadi Sh 50,000 ili watoto waliozaliwa waweze kupata huduma za afya wanapopelekwa hospitali ya wilaya.

Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, kwenye kutoa salamu za serikali katika kikao cha kawaida cha Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rujewa, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Oliva Sule, alisema serikali kamwe haiwezi kufumbia macho jambo hilo.

Alisema serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama italifanyia uchunguzi jambo hilo na kwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa jambo hilo ni kinyume na taratibu za kazi.

"Jambo hili sisi kama serikali hatuna taarifa nalo…kwamba wanawake wanaojifungua nyumbani kwa bahati mbaya kabla ya kufika hosipitali wanapohitaji huduma za chanjo au vipimo kwa watoto wanapowapeleka wanakataliwa na kutozwa elfu hamsini, hatujawahi sikia..nimelisikia hapa na hatuwezi kukaa kimya tutafuatilia, lakinini ni muhimu mkatuletea majina ya hao watu ili tuchukue hatua," alisema Sule.

Pia aliwataka wenyeviti wa vitongoji na wananchi kutolalamika kimya kimya pale wanapoona hawatendewi haki kwenye taasisi za kutoa huduma na badala yake waujulishe uongozi wa juu ili kutatua matatizo ndani ya jamii.

Sule alitoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Muungano, Hawa Msigwa kutoa malalamiko yake baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya utendaji kazi wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji.

Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rujewa, Chameta Godigodi, aliwataka wajumbe kutoa ushirikiano wakati vyombo husika vitakapokuwa vinafuatilia jambo hilo ili kuvirahisishia kazi.

Chanzo: habarileo.co.tz