Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanaochangia ‘earphone’ hatarini kupata fangasi

Earphone Fangasi.png Wanaochangia ‘earphone’ hatarini kupata fangasi

Fri, 16 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na maendeleo ya teknolojia, kumekuwa na uzalishaji wa vitu vingi vinavyorahisisha maisha ambavyo awali havikuwepo, huku wataalamu wa masuala hayo wakiendelea kubuni vipya kila kukicha.

Zamani watu walisikiliza muziki kwa kutumia simu wakiwa wamezishika mkononi, huku sauti ya kinachosikilizwa ikisikika kwa kila mtu.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia, kwa sasa ni nadra kukutana na hilo, kwani wengi hutumia vifaa vinavyojulikana kama spika za masikioni (earphone, headphone na earpod) kwa ajili ya kuzuia sauti ya wanachosikiliza kusikika kwa watu wengine.

Katika matumizi ya vifaa hivyo, kila mtu huwa na sababu zake, huku kukiwa na wale wanaodai wanalazimika kutumia kwa ajili ya kutosumbua wengine.

Mmoja wa watumiaji wa vifaa hivyo kutoka Kigogo, Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake liandikwe, anasema anapenda kuvaa earphone kwa sababu zinamsaidia kusikiliza ujumbe kwa makini bila kelele.

Lakini pia anaeleze anatumia vifaa hivyo kwa sababu anapenda kusikiliza muziki, hasa kutoka kwenye simu yake.

Kwa upande wake, Rajabu Nahemia, mkazi wa Tabata, anasema anapenda kutumia earphone kwa sababu hapendi kusikiliza muziki mbele za watu, kwani muda huo huwa kwenye hisia fulani.

Mbali na kupenda muziki, anasema anavaa earphone aweze kupata ‘testi’ ya muziki anaosikiliza na wakati mwingine anazivaa kwa ajili ya fasheni.

Licha ya mazuri hayo yote, jambo lililozoeleka miongoni mwa watu, hasa wanaokaa pamoja muda mwingi, ikiwemo vyuoni, maofisini na katika shughuli nyinginezo, ni kuazimana vifaa hivi vya masikioni.

Mkuu wa kitengo cha masikio, pua na koo, Dk Bukanu Faustine, kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, anasema baadhi ya watu huazimana earphone bila kujali afya ya masikio ya yule anayemuazima, hali inayomfanya aweke rehani masikio yake.

“Kwa watu wanaopenda kuazimana vifaa hivyo, wapo kwenye hatari kubwa ya kuambukizana ugonjwa wa fangasi kwenye masikio,” anasema Dk Faustine.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa upasuaji wa masikio, pua na koo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk Godlove Mfuko anataja sababu ya maambukizi ya fangasi za masikio, pia hutokea wakati wa kuogelea.

“Fangasi za masikio pia mtu anaweza kuambukizwa wakati wa kuogelea, maji yakiingia masikioni kwa mwenye fangasi hizi, mwingine akija anaweza kupata maambukizi,” anasema Dk Mfuko.

Licha ya watumiaji wa vifaa hivi kuwa na sababu mbalimbali za kuvitumia, Dk Faustine anasema uvaaji wa earphone kwa muda mrefu ni hatari kwa afya ya masikio, kwani kunaweza kuharibu uwezo wa kusikia.

Anashauri watu kutotumia earphone na kama zikiwa na ulazima, wanatakiwa kutumia kwa sauti ya chini sana ambayo haitazuia watu wanaozungumza pembeni kutosikika kwa sababu sauti kubwa huleta athari kwenye masikio.

Mbali na kusababisha matatizo ya masikio, anasema: “Uvaaji wa vifaa hivyo haushauriwi sana kwa sababu unaweza kusababisha ajali kwa mtumiaji endapo akiwa barabarani kwa kutosikia vyombo vinavyopita pembeni yake.”

Anaeleza wapo watu wengi wanaopata shida ya masikio ambao mara nyingi hupatiwa msaada wa mashine za usikivu ambazo zinakuza sauti ili waweze kusikia.

Dk Faustine anasema matatizo ya masikio hayajalishi mtu ametumia earphone kwa siku ngapi au muda gani, kwani kuna mtu anaweza kutumia kwa siku moja lakini kwa sauti ya juu pia anaweza kupoteza uwezo wa kusikia.

Kwa upande wake, Dk Mfuko anasema wanapofanya vipimo hubaini ni namna gani mgonjwa alipata tatizo, iwapo ni kusikiliza sauti kubwa, maambukizi ya fangasi au bakteria.

Licha ya ushauri ambao umetolewa na daktari huyo, kampuni zinazotengeneza vifaa hivyo pia zimekuwa zikijali afya za wateja wao kwa kuweka teknolojia ambayo msikilizaji akiwa anasikiliza muziki kwa sauti ya juu zaidi ya asilimia 50, vifaa hivyo hujishusha sauti na kutoa tahadhari kwa mtumiaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live