Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi kuelimishwa chanjo ya corona

7aa6ab4c0ad6eeabba650d39ea9d5c05 Wananchi kuelimishwa chanjo ya corona

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAIMU Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Ama Kasangala amesema serikali inajipanga kutatoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu na usalama wa chanjo ya virusi vya corona.

Amesema hayo baada ya serikali hivi karibuni kutangaza kuwa Tanzania itatoa chanjo kwa watu wanaohitaji kwa hiyari, ambapo chanjo za aina nne zitaingizwa nchini ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza na HabariLEO jana, Dk Kasangala alisema wapo kwenye mchakato wa kukamilisha taratibu zinazohitajika kabla ya chanjo hizo kuanza kutumika nchini.

“Elimu tutakayoitoa itagusa makundi yote, itagusia umuhimu wa chanjo ili kusaidia taifa kuepuka kupoteza watu kwa maradhi hayo.”

“Lengo ni kuwapa elimu Watanzania kuondokana na dhana potofu kuhusu chanjo inayoenezwa na watu wasio na uelewa wa kutosha,” alisema. Aidha alisema wanaendelea kutoa elimu ya mlipuko wa wimbi la tatu la corona ili wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kama vile kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

“Ujio wa wimbi la tatu la corona ulipoingia nchini, mapokeo yamekuwa madogo na wananchi bado hawana kasi kubwa ya kukabiliana nayo kama hatua ya kuvaa barakoa,

“Wimbi la tatu ni tofauti na yaliyotangulia, kwa sababu linagusa makundi yote ya jamii; wazee, vijana na watoto.

Kwa kuzingatia ukubwa wake, watoto wadogo wanapaswa kukingwa kwa kuepushwa na mikusanyiko na tayari wizara imeshatoa mwongozo wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa, kujihami na maambukizi shuleni,”alieleza.

Alisema elimu pia imeanza kutolewa kwa makundi mbalimbali, yakiwamo ya viongozi wa dini,walemavu,wahudumu wa afya ngazi ya jamii, utengenezwaji wa vipeperushi na miongozo ya afya.

“Watoa huduma za afya hasa vijijini wao wanapita katika maeneo yenyewe mikusanyiko ya watu kama kwenye vituo vya mabasi, masoko na kwenye mikusanyiko ambako wanapita kutoa elimu kwa jamii.

Dk Kasangala alisema wanashirikiana na Chama cha Walemavu Tanzania katika kupata maelezo ya namna ya kufikisha taarifa katika kundi hilo.

“Tayari tumeshachapisha kitabu kimoja cha nukta nundu kwa ajili ya wenzetu wenye ulemavu wa macho ili wapate taarifa kamili ya kujikinga na corona,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz