Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi Ruvuma wajenga kituo cha afya

Kituo Cha Afya Matetereka.png Jengo lililojengwa na Wwananchi kijiji cha Matetereka

Wed, 30 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi wa Materereka katika halmashauri ya wilaya ya Madaba, mkoani Ruvuma wamesema ujenzi wa kituo cha afya kilichojengwa kwa fedha za tozo za miamala umekuwa kama ndoto kwao kwa sababu hawakutarajia kusogezewa karibu huduma za matibabu.

Wananchi walieleza hayo mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmshauri ya Madaba, Sajidu Mohamed aliyefanya ziara ya kukagua mwenendo wa ujenzi wa kituo hicho kilichogharimu Sh250 milioni.

Kituo hicho kimejengwa katika eneo ambalo litasaidia asilimia kubwa ya wananchi wanapata huduma za matibabu kwa urahisi bila kulazimika kwenda maeneo mengine ya jirani.

Constatine Mlelwa alisema wanaona kama ndoto kwa namna walivyokuwa wakihangaika kupata huduma za matibabu, wakilazimika kutumia gharama kubwa kwenda hospitali ya wilaya ya Madaba au mkoani.

“Kwa niaba ya wananchi wa Matetereka tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutujengea kituo cha afya hapa. Kituo hiki kitatumika na wananchi wa vijiji vya Maweso, Matetereka na Mwande kwa sababu hata upasuaji utafanyika hapa,” alisema Mlelwa.

Naye Deograsius Mponda anayeishi Matetereka akiwa na watoto saba, alimshukuru Rais Samia kwa kuwaona kwa jicho la huruma kwa kuwasogezea huduma za matibabu kwa ngazi ya kituo cha afya akisema wamekuwa wakipata adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta matibabu.

“Nina watoto saba lakini natamani nizae mtoto mwingine katika kituo hiki cha jirani maana kipo karibu na makazi yangu. Mungu ambariki Rais Samia kwa moyo wake wa upendo wa kuwajali wananchi mbalimbali hasa wa vijijini.

“Nipo Matetereka tangu mwaka 1992, baadhi ya watoto wangu nilijifungua kwa shida wengine njiani kutokana umbali wa kutembea saa moja kutoka Mwande hadi zahanati iliyopo katika kata hii. Naishukuru Serikali kwa kutusogezea huduma karibu, tena ngazi ya kituo cha afya,” alisema Mponda.

Kwa upande wake, Rogatha Matei mkazi wa kijiji cha Mwande alisema huduma za afya wanapata katika zahanati ya Matetereka lakini wakihitaji matibabu makubwa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 20 hadi Madaba.

“Umbali wake ukipanda pikipiki Sh1,000 hadi halmashauri, tulikuwa changamoto kubwa hasa wajawazito ambapo kama huna fedha huwezi kufika Madaba. Lakini kituo hiki kikikamilika kitakuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Matetereka.

Akizungumzia ujenzi huo, Mkurugenzi Mtendaji, Mohamed alisema ujenzi huo unakaribia kukamilika na kituo hicho kikianza kutoa huduma kitakuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Materereka ambao kwa nyakati tofauti walilazimika kufuata huduma ya matibabu huko Madaba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live