Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wananchi 135,000 wapatiwa chanjo ya UVIKO-19

CHANJO Manyara Wananchi 135,000 wapatiwa chanjo ya UVIKO-19

Fri, 8 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wananchi 135,000 kati ya 669,516 sawa na asilimia 30 wa Wilaya tano za Mkoa wa Manyara, wamepatiwa chanjo ya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19

Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, (RMO) Dkt Damas Kayera anasema hadi hivi sasa watu 135,000 wa mkoa huo wameshapatiwa chanjo ya UVIKO-19 na wanatarajia hadi mwishoni mwa mwaka huu lengo la wananchi 669,516 kupatiwa chanjo litafikiwa.

Dkt Kayera anasema kwamba hivi sasa wananchi wa Manyara, wamepata mwamko mpya kwani wameshiriki mno katika kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 tofauti na hapo awali.

“Tupo sehemu nzuri kwani hadi hivi sasa tumefikia asilimia 30 kutoka asiliamia 3.7 mwaka jana ila lengo ni kufikia asilimia 40 hadi mwishoni mwa mwezi Julai na kufikia asilimia 70 mwezi Desemba mwaka huu,” anaeleza Dkt Kayera.

Anasema kuwa wanatarajia kufikisha malengo hayo kutokana na mwamko wa elimu ya kupata chanjo ya UVIKO-19 waliyonayo wananchi wa halmashauri saba za wilaya tano za mkoa huo.

Mkazi wa Kata ya Bagara Wilaya ya Babati, Rose Justin anasema wananchi wa mkoa huo wamehamasika kupata chanjo mara baada ya kuona baadhi ya waliokumbwa na janga la UVIKO-19 walivyoteseka.

“Awali elimu ilikuwa haijawanufaisha watu wengi ila baada ya kuona kuwa unaweza kupata UVIKO-19 ila ikiwa umepata chanjo ambayo haina malipo, haupati athari kubwa kwenye changamoto ya kupumua,” anaeleza Rose.

Mkazi wa Kata ya Sanu Wilayani Mbulu, Benedict Bilauri anaeleza kuwa hivi sasa wananchi wengi wamehamasika kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 kutokana na hali iliyojitokeza mwaka jana kwani kuna baadhi ya watu walipata changamoto ya kupumua.

“Hali ilikuwa mbaya kwani matukio ya vifo vilivyotokana na changamoto ya kupumua yaliathiri watu wengi hivyo ikasababisha wananchi kupata chanjo ili kujihadhari na janga hilo,” anasema Bilauri.

Anasema elimu waliyopatiwa na ushuhuda uliotokea umechangia kwa kiasi kikubwa kuwapa msukumo wananchi wa Mbulu kupatiwa chanjo ya maambukizi ya UVIKO-19.

“Mwaka jana hali ilikuwa mbaya na ilisababisha hadi mbunge wa jimbo la Mbulu mjini Paul Zacharia Isaay, azungumze Bungeni na kufikisha kilio cha changamoto ya vifo vinavyotokana na kupumua,” anaeleza Bilauri.

Katibu mkuu msaidizi na mratibu wa kimataifa wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 wa shirika la Afya duniani (WHO) Ted Chaiban akizungumza hivi karibuni mjini Babati alipofika kuhamasisha chanjo hiyo ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kupambana na UVIKO-19.

Chaiban anaeleza kuwa Tanzania ilikuwa nyuma katika utoaji wa chanjo ila hivi sasa kuna mabadiliko makubwa kwani muamko umeongezeka kutoka asilimia 6.3 ya utoaji wa huduma ya chanjo ya UVIKO-19 na kufikia asilimia 12.4.

“Nawapongeza wauguzi na wahudumu wa afya kwa kuendelea kutoa huduma ya chanjo ya UVIKO-19 ikiwemo utoaji wa elimu kwani inasaidia kuongeza idadi ya watanzania kupata huduma,” anasema.

Anaeleza kuwa kutokana na hali hiyo kunaonekana manufaa makubwa na pia jitihada za Serikali katika kuwalinda wananchi wake kujiepusha na magonjwa mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live