Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi wajengewe mbinu kukabiliana na unyanyasaji kijinsia

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Femina Hip, Dk Minou Fuglesang amesema ni muhimu kwa wanafunzi kuendelea kujengewa uwezo wa kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyoendelea kutokea nchini.

Ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 29, 2018 wakati wa kusaini makubaliano kati ya Femina na Serikali ya Sweden ambapo jumla ya Sh4.5 bilioni zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza mpango mkakati wa Femina wa mwaka 2018/20.

Mkurugenzi huyo amesema watoto wanakumbana na changamoto nyingi ikiwamo mimba na ndoa za utotoni ambazo zinakwamisha ustawi wao kielimu na kiuchumi.

"Nafasi yetu kubwa tuliyonayo ni kuwajengea uwezo vijana mashuleni juu ya namna bora ya kujikinga na vitendo vya unyanyasaji pamoja na kuwahimiza kupenda masomo ili wasishawishike kwa urahisi," amesema.

"Elimu ina nguvu ya kuwafanya vijana wetu kuwa salama, tunawajengea uwezo wa kujitambua pamoja na kujua haki ya uhuru wa kuchagua," amesema.

Amesema kuna matokeo chanya ya uwepo wa Femina hasa mashuleni kwa kuwa vijana wengi wanaonekana kutambua nafasi zao katika kujenga jamii bora pamoja na kujikwamua kiuchumi.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano na Maendeleo wa ubalozi wa Sweden hapa nchini, Ulf Kallstig amesema ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za maendeleo unatakiwa kupewa kipaumbele ili nchi iweze kuvifikia vipaumbele vyake ikiwamo uchumi wa Kati.

"Vijana wana jukumu muhimu katika kuiendesha Tanzania kuelekea taifa la uchumi wa Kati wa Viwanda, ni muhimu kwetu kuzishirikisha sauti za vijana katika mijadala ya kimaendeleo," amesema.

Shirika hilo limeweza kufikisha jumla ya Vikundi (Clubs) 2,340 kwenye shule za sekondari na vyuo ambapo kwa miaka 20 limekuwa likitoa elimu ya uzazi na haki pamoja na uwezeshaji kiuchumi kwa vijana.

Chanzo: mwananchi.co.tz