Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliowekewa nyonga na magoti bandia Mloganzila waanza kuruhusiwa

Waliowekewa Nyonga Na Magoti Bandia Mloganzila Waanza Kuruhusiwa.jpeg Waliowekewa nyonga na magoti bandia Mloganzila waanza kuruhusiwa

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kuweka magoti na nyonga bandia katika kambi maalumu inayoendelea Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila wameanza kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya afya zao kuimarika.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo leo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji MNH-Mloganzila Dkt. Godlove Mfuko ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji amesema kuruhusiwa kwa wagonjwa hao kunadhihirisha namna Mloganzila ilivyokidhi viwango vya kimataifa vya kufanya aina hiyo ya upasuaji.

“Kwa viwango vya kimataifa mtu aliyefanyiwa aina hii ya upasuaji kama hakuna dharura yoyote huwa ni siku tatu hadi tano, kwa hiyo na sisi tunakwenda na viwango hivyo ambapo wagonjwa walifanyiwa jumatatu leo wanaruhusiwa”

Dkt. Mfuko amebainisha kuwa mbali na kupata wagonjwa kutoka karibia mikoa yote ya Tanzania, pia alipatikana mgonjwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), jambo ambalo linaonyesha kuwa kambi siyo tu imenufaisha watanzania bali hata raia kutoka nchi ya kigeni.

Kwa upande wake kiongozi wa kambi hiyo Prof. Mamoun Gadir kutoka Hospitali ya Queen Elizabeth nchini Uingereza amesema kuwa mpangilio na muundo wa hospitali ya Mloganzila hauna tofauti za hospitali za nchi zilizoendelea na kwamba wataalamu wanayo maarifa ya msingi hivyo wakiongezewa maarifa za ziada kidogo tu wanaweza kuwa wabobezi.

Aidha ameshauri Hospitali ya Mloganzila kuwa kituo maalumu cha kutoa matibabu ya ngonya na magoti.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Nyonga na Magoti MNH-Mloganzila Dkt. Shilekilwa Makira amebainisha sababu mbalimbali zinazopelekea maradhi ya nyonga na magoti kuwa ni pamoja na umri mkubwa, maradhi ya Selimundu, Pumu ya Mifupa na Ajali.

Amesema kuwa kambi hiyo mbali na kutoa huduma pia imetoa fursa kwa wataalamu kutoka hospitali za Temeke RRH, CCBRT na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH) kujifunza, pia ametoa shukrani kwa wataalamu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushiriki kuwajengea uwezo.

“Baada ya kambi kuisha utaratibu wa matibabu kwa watu wenye changamoto za nyonga na magoti utaendelea kama kawaida ambapo tutawaona katika kliniki zetu na kama wataonyesha wanahitaji upasuaji tutawafanyia,” amesema Dkt. Makira

Chanzo: www.tanzaniaweb.live