Huduma ya upandikizaji uume iliyofanywa kwa wanaume wawili waliokuwa na tatizo la nguvu za kiume katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma, imeonesha matokeo mazuri na ‘heshima’ imerejea kwa familia zao, huku gharama zake zikiwa kati ya Sh. milioni sita hadi 10.
Akizungumza jijini hapa na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya hospitali hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk. Alphonce Chandika, alisema huduma hiyo imeanzishwa baada ya kubaini kuna tatizo kubwa la nguvu za kiume.
“Tumeona hata wenzetu waganga wa kienyeji wanapita huko mtaani kule na dawa ya kutibu tatizo hili. Wananchi wanasumbuka, sisi kama taasisi ya umma tumeona tuje na mkakati wa kuwasaidia wananchi.
“Tulianza kutoa huduma mwezi Juni 2022 kwa wanaume wawili, lakini kwa habari njema kutoka kwao mambo ni mazuri.
“Mambo ni mazuri sana kwa sababu tuliwapa masharti wakae wiki sita ndipo waanze kujaribu mitambo, mitambo imekaa vizuri na wao wametuambia matokeo mazuri wamefurahi sana na imerejesha heshima katika familia zao,” alisema.
Alibainisha kuwa wako katika mchakato wa kuongeza wigo wa utoaji huduma ili zipatikane kwa wahitaji wote na wale wanaotengeneza vipandikizi wanakamilisha taratibu za usajili ili kufungua ofisi Dar es Salaam itakayorahisisha upatikanaji wake.
“Ninatumaini baada ya kuanza sisi na hospitali zingine zitatoa kwa kuwa uhitaji ni mkubwa. Sisi pekee yetu hatutotosheleza. Kwa hiyo, tutashirikiana na wenzetu hata kuwapa mafunzo ili watoe huduma katika hospitali zao,” alisema.
Kiongozi huyo alisema gharama siyo kubwa kulinganishwa na tabu anazopata mtu mwenye tatizo hilo. Ni kati ya Sh. milioni sita na 10.
Alisema magonjwa ya kisukari na shinikizo yanachangia kwa kiasi kikubwa tatizo la nguvu za kiume na kuwashauri wananchi kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Pia nitahadharishe kuhusu mitindo ya kujamiana ambayo imeonekana kuchangia tatizo hili kama mlivyosikia kuna mmoja wa wagonjwa ilitokana na mitindo hiyo (sehemu zake za siri zilivunjika). Sasa inawezekana kuna wengine huko wengi mtaani, hivyo nitoe tahadhari,” alisema. Kuhusu upandikizaji figo, kiongozi huyo alisema kwa mwaka uliopita wananchi wanane walinufaika na upandikizaji figo na wametumia Sh. milioni 288.
Kama wangepelekwa nje ya nchi kupata huduma hiyo, wangetumia Sh. milioni 600 kulingana na gharama za hospitali za nje, hivyo kwa huduma hiyo serikali imeokoa Sh. milioni 312.
“Katika huduma za matibabu ya moyo tumeendelea kuimarika. Mwaka uliopita tumefanya uchunguzi wa mishipa ya moyo kwa wagonjwa 320, upandikizaji betri wagonjwa 13, watoto waliozibwa matundu katika moyo 14, kuweka vizibua njia ya mishipa ya moyo 54, huduma ya vipandikizi katika magoti na nyonga wananchi 72 wamenufaika na huduma hii na serikali imetumia Sh. milioni 864 na kama wangeenda kupata huduma hii nje ya nchi, ingeigharimu serikali Sh. bilioni 2.5, hivyo Sh. bilioni 1.638 zimeokolewa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika huduma ya upandikizaji uloto, imekuwa na manufaa makubwa kwa watoto wanne ambao wamepona kabisa na huduma hiyo inapatikana Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa gharama za matibabu Sh. milioni 50 wakati matibabu hayo nje ya nchi yanagharimu Sh. milioni 120 hadi 135.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2023/24, wametenga Sh. bilioni 64.52. Kati yake, Sh. bilioni 18.62 ni za miradi ya maendeleo ili kuendelea kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri mbali kupata matibabu.
Alisema miradi yao inajumuisha ujenzi wa kituo cha upandikizaji wa figo chenye vyumba vya upasuaji kwa anayechangia figo na anayepokea.