Hospitali ya Taifa Muhimbili itaendelea kuongeza huduma za kibingwa bobezi ili kuendelea kuwahudumia watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi hatua itakayo endeleza kuchochea utalii tiba hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Muhimbili Dkt. Rachel Mhaville wakati akizunguza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi, kuhusu huduma ya matibabu kwa njia ya hewa tiba yenye mgandamizo wa oksijeni (Hyperbaric Medicine Treatment), ambapo wanufaika wa huduma hiyo wamepata fursa ya kutoa ushuhuda juu ya matibabu waliyoyapata na afya zao kuimarika.
Dkt. Mhaville amesema MNH ni hospitali ya kwanza ya Umma nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutoa huduma hiyo na kwamba imekua na matokeo mazuri.
“Leo tuna mashuhuda wawili ambao walikuwa na vidonda kwenye miguu yao kwa miaka mingi ila baada ya kuja Muhimbili na kupatiwa matibabu kwa kutumia mtambo huu sasa wamepona” ameeleza. Dkt. Mhavile
Mmoja wa mashuhuda hao Bw. Hassan Kindamba ambaye alikuwa na kidonda kwa zaidi ya miaka 11 amesema kidonda hicho kilikuwa kinamsababishia maumivu makali na alikuwa hawezi kupata usingizi kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Naye Bw. Innocent Masali ambaye pia alikuwa na kidonda kilichomsumbua kwa miaka minne ameeleza kuwa alizunguka hospitali mbalimbali kutafuta msaada bila mafanikio ila baada ya kuja Muhimbili na kupatiwa matibabu kwa njia hiyo amepona.
Baadhi ya wagonjwa wanaoweza kunufaika na huduma hiyo ni wenye vidonda sugu, wagonjwa wa kisukari, walioathirika na moshi baada ya kuungua na moto, wenye saratani wanaopata changamoto ya mionzi, wanaopata changamoto ya hewa ya oksijeni ,wanaozama baharini na wagonjwa wenye changamoto ya ugonjwa wa Seli Mundu.