Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi zaidi ya 300 Mirerani wapewa huduma ya macho bure

16760 Pic+macho TanzaniaWeb

Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mirerani. Zaidi ya wakazi 320 wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamepewa huduma ya afya kwa kupimwa na kupewa matibabu bure kwenye shule ya msingi ya Blue Tanzanite.

Mkurugenzi wa shule ya Blue Tanzanite, Raphael Ombede akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 11 amesema huduma hizo zinatolewa bila malipo kwa muda wa siku tatu shuleni hapo.

Amesema bila kuwa na afya nzuri huwezi kuzalisha uchumi hivyo wananchi wanatakiwa kufika na kupata huduma za kupima afya ili wapate matibabu bila malipo.

Amesema vifaa vya kutosha vipo ikiwemo chumba cha maabara, vipimo, dawa na ushauri nasihi kwa hiyo wananchi wajitokeze kwa wingi ili kupata huduma mbalimbali.

"Suala la kutokutambua lugha ya kiingereza lisiwape hofu wahusika kwani kuna watu ambao ni maalum kabisa kwa ajili ya kutafsiri na kupatiwa huduma," amesema Ombade.

Mmoja kati ya wakazi wa mtaa wa Songambele, Milton Rohbi, alisema yeye na mke wake na watoto wao wawili wamepatiwa huduma ya vipimo na matibabu bila kutozwa fedha.

Rohbi amesema mara baada ya kupata taarifa ya kutolewa huduma hiyo bila malipo alifika na familia yake ili kupima afya kwani binadamu kwa kawaida huwa anatembea na maradhi mengi.

Mkazi wa mtaa wa Kazamoyo, Anna Monko amesema amepimwa macho na kupewa miwani ambayo itamsaidia hasa wakati wa kusoma kwani alikuwa anatoa machozi pindi akishika kitabu.

Monko amesema anawashukuru madaktari hao na wahusika wote waliofanikisha uwepo wao hadi wananchi wa mji mdogo wa Mirerani wakanufaika na fursa hiyo.

Mchungaji Abraham Stanslaus wa Baptist Church Oloirien, amesema huduma hiyo imewezeshwa na Oloirien Community Clinic ya jijini Arusha, inayotoa huduma ya afya na elimu.

Stanslaus amesema wanatoa huduma ya vipimo mbalimbali ikiwemo homa ya malaria, shirikisho la damu, meno, macho, homa ya matumbo na magonjwa ya maambukizi.

Chanzo: mwananchi.co.tz