Dar es Salaam. Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wametakiwa kuongeza kasi ya kufanya usafi wa mazingira na kuondoa mazalia ya mbu ili kupunguza uwezekano wa kuhifadhi mbu wenye vimelea vya Dengue.
Aidha, wametakiwa kuwahi hospitali na kwenye vituo vya afya pale wanapohisi mabadiliko kwenye miili yao ili wafanyiwe uchunguzi wa kitabibu kwani katika hospitali za Serikali kipimo cha Dengue ni bure.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi Mei 11 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Yudas Ndungile wakati akihojiwa na kituo cha radio cha Clouds Fm.
Dk Ndungile amesema kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo imekuwa kubwa katika jiji hilo hasa wilaya za Ilala, Ubungo na Kinondoni.
Amesema hadi sasa takwimu zinaonyesha watu wasiopungua 1,000 wameugua ugonjwa huo katika jiji la Dar es Salaam tangu ulipotokea mlipuko Januari 2019.
“Jambo la muhimu ni kusafisha mazingira, nasisitiza kinga ni bora kuliko tiba tuondoe mazalia ya mbu katika maeneo yanayotuzunguka na zile sehemu tunapenda kukaa.”
Habari zinazohusiana na hii
- Serikali yashusha gharama za vipimo vya dengue nchini
- Dar yaanza kunyunyizia viuadudu kudhibiti dengue
- Dar, Tanga watakiwa kuvaa nguo ndefu kuepuka Dengue
“Kingine ni kuvaa mavazi yatakayofunika mwili hasa kwenye mikono na miguu, hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kwamba ukipaka mafuta ya nazi mbu wa Dengue hawatakufuata.”
Dk Ndungile pia amesisitiza watu kuwahi hospitali na kwenye vituo vya afya pale wanapohisi mabadiliko kwenye miili yao ili wafanyiwe uchunguzi wa kitabibu.
Kuhusu gharama za vipimo amesema katika hospitali za Serikali kipimo cha Dengue ni bure.