Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Arusha wakumbwa na ugonjwa wa kuhara, kutapika

46347 Pic+arusha Wakazi Arusha wakumbwa na ugonjwa wa kuhara, kutapika

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Ugonjwa wa kuhara na kutapika umewakumba baadhi ya wakazi wa jiji la Arusha wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari.

Diwani wa Daraja mbili (CCM) kata ambayo ndiyo ina wagonjwa wengi, Prosper Msofe amesema wanahisi chanzo cha kusambaa ugonjwa huo ni mwingiliano wa mabomba ya maji safi na maji taka katika jiji la Arusha.

"Mimi na familia yangu tumekumbwa pia na ugonjwa huu na niliwapigia watu wa idara ya maji wakaja nyumbani kupima maji, lakini bado tatizo lipo kata nzima, watu wanahara na kutapika tunaomba Serikali iingilie kati," amesema leo Jumanne Machi 12, 2019 alipozungumza na Mwananchi.

Muuguzi mfawidhi wa kituo cha afya Daraja la mbili, Nyandaro Maagi amesema ndani ya siku tatu wamepokea wagonjwa zaidi ya 92 ambao walikuwa wamefika katika kituo hicho kwa matatizo hayo.

"Tulipokea wanafunzi kama 66 wa Shule ya Sekondari ya Felix Mrema, wengine 26 wa Sinoni Sekondari na wanafunzi kama 10 wa Islamic Girls na watu wazima baadhi tuliwapatia matibabu na wameruhusiwa na wengine walikuwa na hofu tu baada ya kuharisha mara moja ama mbili," amesema.

Mganga mfawidhi katika kituo cha afya Revolosi, Antony Mmao, amesema kituo hicho kimepokea wagonjwa 15 juzi na jana na wote wamepatiwa matibabu.

"Ni kweli kuna tatizo la ugonjwa wa kuhara na kutapika, binafsi kwa wiki nzima nilikuwa nasikia mitaani lakini tumeanza kupokea wagonjwa ambao wanadai kunywa maji ambayo si masafi," amesema.

Kelvin Zebedayo, mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Moshono na Joshua Aloyce mwanafunzi wa Shule ya Msingi Uhuru, wakazi wa Daraja mbili, wameeleza kushindwa kwenda shule kutokana na kuumwa tumbo la kuharisha na kutapika.

"Mimi nilikuwa shuleni jana na wenzangu, tulianza kuharisha na kutapika shuleni, wakaitwa wazazi na tukapelekwa hospitali ya Kaloleni," amesema Zebedayo.

Aloyce amesema baada ya juzi kutoka shule alikunywa maji ya bomba na kuanza kuumwa tumbo kisha kuharisha na kutapika. "Sijaenda shule kwa sababu naumwa na pia kuna wenzangu wengine wanaumwa," amesema.

Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Arusha (Auwsa), imekanusha bomba za maji safi kuingiliwa na mfumo wa maji taka kama ambavyo wananchi wengi wamekuwa wakidai.

Ofisa uhusiano wa Auwsa, William Shayo amesema baada ya kupata taarifa za bomba za maji safi kutoa maji taka, walifuatilia na kuchukua sampuli za maji na kwenda kupima katika maabara na hawakuona tatizo.



Chanzo: mwananchi.co.tz