WAJAWAZITO katika kata ya Kwaga Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wanalazimika kuzalishwa na wakunga wa jadi kwa sababau ya upungufu wa wauguzi na wakunga katika zahanati hiyo ambayo inatajwa kuwa na watumishi wawili.
Zahanati hiyo hiyo ina mganga mmoja pamoja na mfamasia hali ambayo inahatarisha afya ya mama na mtoto wakati wakujifungua.
Nipashe imeongea na mmoja ya mkunga wa jadi, Joyce Nzila, ambaye mara kadhaa amekuwa akizalisha wajawazito katika zahanati hiyo kutokana na mganga kuwa na majukumu ya kuhudumia wagonjwa wengine au akiwa nje ya kituo cha kazi.
"Sisi haturuhusiwi kuzalisha, lakini unafika zahanati unakuta mganga anatibu mgonjwa huwezi kumuacha mjamzito inabidi tu uzalishe , sasa tunaomba tusaidiwe tupate wauguzi ili tupumzike kufanya majukumu yasiyo yetu,’’ amesema.
Nzila amesema wanaomba serikali ifanye utatuzi wa haraka wa jambo hilo ili wakunga wajadi waachane na majukumu ya kuzalisha wajawazito badala yake waendelee kuwahamasisha wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuwasindikiza.
Amina Mohamed amasesema zahanati hiyo, hususani wodi ya wazazi haikidhi mahitaji yao kwani chumba ni kidogo ambacho kina vitanda viwili vya wajawazito vya kujifungulia hivyo, wanaomba serikali kufanya utaratibu wa kupanua wodi ya wazazi na kuongeza vitanda ili kuondoa usumbufu wanaoupata.
Ameeleza hali hiyo imekuwa ikisababisha wajawazito kupatiwa rufaa za kwenda kwenye kituo cha afya Rusesa wakati kunapokuwa na wajawazito wengi wanao karibia kujifungua katika zahanati hiyo.
Kutokana na hali hiyo ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu wengine wamekuwa wakijifungulia njiani wakati wakisafirishwa.
Akitoa majibu ya malalamiko hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Joseph Kashushura, ameeleza uwepo wa upungufu wa watumishi wa afya zaidi ya asilimia 65 ambao umegusa karibu kila sehemu ya kutolea huduma za afya jambo ambalo linasababisha baadhi ya huduma kutokufanyika kikamilifu.
Ameahidi kufuatilia jambo hilo kwa ukaribu na endapo itabainika kuwa kuna uhitaji zaidi ya maeneo mengine ya halmashauri hiyo hatua za haraka zitachukuliwa ikiwemo kuchukua watumishi katika maeneo mengine yasiyo na uhitaji mkubwa na kuwapeleka katika zahanati hiyo.
"Ngoja nilifuatilie nijue nikiona tatizo ni kubwa sana kuliko maeneo mengine , tutachukua mtumishi hata mmoja sehemu nyingine tupeleke pale kufanya kazi hata kwa muda," amesema Kashushura.