Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajawazito wanaohudhuria kliniki waongezeka

8653a149398bf6ebc5bd91cc548eabc8 Wajawazito wanaohudhuria kliniki waongezeka

Sat, 29 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imefanikiwa kuongeza idadi ya wajawazito wanaohudhuria kliniki kutoka wanawake 16,494 mwaka 2018/2019 hadi kufikia 32,103 mwaka 2019/2020.

Mafanikio hayo yanatokana na halmashauri hiyo kujikita kwenye utekelezaji wa Sera ya kuboresha huduma za uzazi na mtoto hasa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, ikiwa ni pamoja na kutekeleza malengo ya Milenia kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na hamasa kubwa iliyowafikia wananchi na hivyo kutambua umuhimu wa wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito wake kadiri anavyoshauriwa na wataalamu.

Msangi alisema kwa upande wa huduma ya uzazi ya wanawake wajawazito waliojifungulia katika vituo vya huduma idadi pia imeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambayo wengi wao walikuwa wakijifungulia majumbani na kwa wakunga wa jadi.

Alisema matokeo ya mafanikio hayo yamekuwa ni pamoja na kupungua kwa vifo vya wanawake vitokanavyo na matatizo ya uzazi ambapo kwa mwaka 2019/2020 kati ya wanawake 11,743 waliojifungua ni wanawake watatu pekee walipoteza maisha kiwango alichosema kimepungua kwa kasi kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Msangi pia alisema katika kipindi hicho pia halmashauri hiyo imefanikiwa kufikia lengo la kitaifa la kiwango cha chanjo cha asilimia 95 ambapo yenyewe imefikia asilimia 90 na kuongeza kuwa wanaamini hawakuweza kuvuka lengo la kitaifa kutokana na makadirio makubwa waliyopewa tofauti na uhalisia ulivyo japo pia uelewa katika jamii kuhusu umuhimu wa chanjo umeongezeka na wengi wanapeleka watoto kupata chanjo.

Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbarali, Godfrey Mwakalila alisema mwamko wa jamii katika kuzingatia mahudhurio ya kliniki na pia kwenda kupata huduma za msingi ikiwemo kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma unatokana pia na mazingira rafiki yaliyowekwa hasa na serikali kwa kuboresha miundombinu.

Aliyekuwa diwani wa kata ya Luhanga, Dira Funika alisema wajawazito na jamii kwa ujumla hivi sasa wanashawishika kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma baada ya kuona ni mazingira rafiki na yanayolenga kuokoa afya za wajawazito na watoto wanaozaliwa.

Chanzo: habarileo.co.tz