Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajawazito walalamikia kukosa faragha

29805 WAJAWAZITO+PIC TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Baadhi ya wanawake wanaojifungua katika Zahanati ya Tabora Mjini wamelalamikia ukosefu wa uzio kuwa unawakosesha faragha ya kutosha.

Kwa mujibu wa wakazi wa mjini hapa, kukosekana kwa uzio na mapazia huwapa urahisi wapita njia kuwaona wajawazito wanapokuwa katika harakati za kuelekea kujifungua.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mwanne Mchemba alisema hayo wakati akikabidhi mifuko 50 ya saruji na mashuka 20 kwenye zahanati hiyo na akasisitiza kuwa sehemu hiyo ni muhimu kuwa na uzio ili kuwawekea faragha wajawazito.

Mbunge huyo alisema wakati mjamzito anapopatwa na uchungu anaweza kufanya jambo lolote ambalo si la kawaida kama kukimbia ovyo au kuvua nguo, hivyo akataka ujenzi wa uzio kupewa kipaumbele ili mambo yanayoendelea ndani yasionekane kwa wapita njia.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Tabora, Ponda Dunduma alisema wanawake wanaokwenda kujifungulia katika zahanati hiyo huwa na wakati mgumu kutokana na kutokuwepo na uzio.

Alimshukuru mbunge huyo kwa msaada wake na kwamba wataanza kujenga uzio kwenye eneo lenye barabara ya Madaraka na upande wa Soko Kuu la Tabora.

Zahanati hiyo inatumiwa na wakazi wa Kata ya Chemchem kwa ajili ya matibabu na wajawazito wanaotaka kujifungua.



Chanzo: mwananchi.co.tz