Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajawazito walalamika kujifungulia nje ya zahanati

Wajawazito Pic Data Wajawazito walalamika kujifungulia nje ya zahanati

Wed, 2 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Baadhi ya wanawake wajawazito katika kata ya Kidahwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wamelalamikia kujifungulia nje ya zahanati ya kata hiyo wakidai kuwa hali hiyo inatokana na wahudumu wa zamu kutokuwepo muda wa usiku.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano Februari 2, 2022 wamesema wamekuwa wakipata changamoto hiyo ambayo imepelekea baadhi yao kupoteza maisha kwa kukosa huduma.

Mkazi wa kijiji cha Kidahwe, Sheila Omary amesema alinusurika kifo baada ya kushikwa na uchungu usiku wa saa saba Januari 17, 2022 na alipofika katika zahanati alikuta imefungwa na walipojaribu kumpigia mhudumu wa zamu aliyekuwepo siku hiyo ambaye ni mganga mfawidhi wa zahanati hiyo simu yake iliita bila kupokelewa.

Amesema alilazimika kujifungulia sakafuni nje ya zahanati hiyo huku akisaidiwa na wakunga wa jadi na baada ya kujifungua alikuwa akitokwa na damu nyingi huku viongozi na baadhi ya wananchi wakiendelea kumtafuta mhudumu wa zamu huyo ambaye kwasasa anaishi mjini.

“Tatizo langu sio mara ya kwanza kutokea wanawake wanalalamika na nimeona wamepatwa na tatizo hili jambo ambalo linahatarisha maisha ya mjamzito na mtoto, kwani wakati mwingine akipigiwa simu anasema wazalishwe na wakunga wa jadi,” amesema Sheila.

Mwenyekiti wa kamati ya afya kata ya Kidahwe, Shahadu Dioya amesema matukio ya wanawake wajawazito kukosa huduma nyakati za usiku katika zahanati hiyo yamekuwa mengi na tayari tumeshakaa vikao na kulifikisha kwa viongozi wa juu cha kushangaza hadi wakati huu hakuna hatua zilizochukuliwa na hali bado inaendelea.

Diwani wa kata ya Kidahwe, Heri Kigufu amesema amekuwa akipokea malalamiko hayo kutoka kwa wananchi wake mara kadhaa na wamekuwa wakizungumza naye mara kwa mara kuhusiana na malalamiko hayo na kukiri kosa na kuomba msamaha lakini amekuwa akiendelea.

“Nilienda kulalamika kwa mganga mkuu wa wilaya (DMO), na alikiri kupitia kwenye baraza la madiwani na kusema amemuagiza mganga mfawidhi wa zahanati hiyo watengeneze zamu na kuhakikisha kila siku ya kazi asikosekane mtumishi kwenye kituo cha kazi lakini utekelezaji haupo,” amesema Diwani Kigufa.

Akifafanua jambo hilo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Lusajo Mwakajoka amekiri kupokea malalamiko hayo na kuwepo kwa tatizo hilo mwezi Januari la mama kujifungulia sakafuni.

Amesema walifatilia na kumtaka mganga mfawidhi huyo kutoa maelezo ya tukio zima lilivyokuwa, na kwamba changamoto iliyopo sasa hakuna nyumba ya watumishi pale na mganga anaishi mjini lakini baada ya tukio hilo alitoa maelekezo ya kukaa karibu na zahanati hiyo ili wananchi waweze kupata huduma.

Amesema halmashauri tayari imepokea Sh90 milioni kwaajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi wa zahanati hiyo, na kwamba ujenzi unatarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa maana taratibu zote za awali za ujenzi zimeshakamilika.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz