Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajawazito huenda wodini na mitishamba

56598 PIC+WAJAWAZITO

Fri, 10 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Baadhi ya wajawazito wilayani Sengerema huenda hospitali na dawa za mitishamba wakati wanapokaribia kujifungua, hali ambayo madaktari wanasema inaweza kuwasababishia vifo au kutopata watoto baadaye.

Hali hiyo imebainika wakati Serikali ikiendelea kuhimiza huduma salama za afya ya uzazi kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Mshauri wa afya wa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, Modesta Masala alisema juzi kuwa kinamama wanaojifungua hukutwa wameficha dawa za mizizi ambazo wanaamini huongeza uchungu na hivyo kuwawezesha kujifungua haraka, lakini dawa hizo pia hutumiwa na wengine kuharibu mimba changa.

Takwimu zilizotolewa na ofisi ya mganga mkuu wa Wilaya ya Sengerema zinaonyesha kuwa mwaka 2018 kulikuwa na matukio 552 ya mimba kuharibika wakati mwaka uliotanguliwa yalikuwa 612.

Hata hivyo, takwimu hazionyeshi kama baadhi ya matukio hayo yalisababishwa na matumizi ya dawa za mitishamba.

Pia, takwimu hizo zinaonyesha kuwa tatizo la kuharibika kwa mimba ni la pili kwa ukubwa katika hospitali hiyo baada ya malaria.

Masala alisema wanazo dawa za mitishamba walizozikuta kwa kinamama waliokwenda kujifungua.

“Mara kadhaa tunawakuta nazo wodini wanapokuja kujifungua,” alisema.

“Wanadai wamepewa na waganga wao huko mitaani na wakati mwingine wanagawiana humo humo wodini.

“Dawa hizo za asili zipo za ungaunga, za mizizi na wakati mwingine za majimaji, ndizo zinazotumika na baadhi ya wasichana kutoa mimba, ingawa ni vigumu kukiri kuwa (wasichana hao) wametoa mimba kwa makusudi.”

Akizungumzia kuhusu matumizi ya dawa za kienyeji, mratibu wa afya wa wilaya, Maria Mgoa alisema matumizi ya dawa hizo yana madhara.

“Madhara ya hili ni makubwa,” alisema.

“Wapo wanaopasuka kizazi kwa sababu ya dawa hizo za kusababisha uchungu mkali katika kipindi kifupi. Pia husababisha mtoto kuzaliwa akiwa amekufa.”

Mgoa alisema mara kadhaa mwanamke anapokwenda hospitalini hapo akiwa na tatizo la mimba kuharibika, wauguzi huangalia kwanza suala la kuokoa maisha yake kwanza.



Chanzo: mwananchi.co.tz