Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waishio vijiji vya pembezoni waomba uboreshaji huduma

B581aea2d5a89cb252d215d98921c912.jpeg Waishio vijiji vya pembezoni waomba uboreshaji huduma

Fri, 20 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WANANCHI wanaoishi vijiji vya pembezoni wilayani Tunduru, wameiomba serikali kuboresha na kuwekeza nguvu kubwa kwenye huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo kuondokana na kero ya upatikanaji wa huduma hizo.

Wamesema kwa sasa bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma katika maeneo hususani ya vijijini kama maji, vifaa tiba na dawa kwa wananchi wanaobainika kupata ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na magonjwa mengine.

Wametoa maombi hayo kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni ya uelimishaji, uhamasishaji na uchunguzi wa ugonjwa wa TB katika kijiji cha Likweso kata ya Mchoteka kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji iliyofanywa na Kitengo cha Kifua Kikuu na Ukoma Hospitali ya Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma.

Mmoja wa wakazi wa wilaya hiyo, Andrew Titus amewaomba wataalamu wa afya kujikita zaidi katika maeneo hayo kwa ajili ya kutoa elimu kwani kuna watu wengi wanaougua kifua kikuu lakini kutokana na kukosa elimu wameshindwa kwenda hospitali kupata tiba sahihi, jambo linalochangia kupoteza nguvu kazi ya taifa na kuongezeka kwa umaskini katika jamii.

Naye Iman Masota amesema vijiji vilivyopo pembezoni bado kuna changamoto kubwa ya kufikiwa na baadhi ya huduma za kijamii kama maji safi na salama, huduma za afya na miundombinu ya barabara na umeme, hivyo jamii kukosa uelewa kuhusiana na masuala mbalimbali.

Mwananchi mwingine, Mwarabu Issaya ameomba kudhibiti unywaji holela wa maziwa ya ng’ombe yasioandaliwa vizuri ili kudhibiti uwezekano wa kuenea kwa ugonjwa huo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wa Hospitali ya Wilaya Tunduru, Dk Mkasange Kihongole alisema kwa sasa msisitizo mkubwa wa Hospitali ya Wilaya Tunduru ni kuwatumia wataalamu wake kwenda vijijini kwa ajili ya kuhudumia wananchi na kuwaanzishia tiba wale watakaobainika kuwa na maradhi, badala ya wa wataalamu kukaa ofisini.

Akizungumzia juu ya ugonjwa wa kifua kikuu, Dk Kihongole alisema lengo la Serikali ya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2035 ugonjwa wa kifua kikuu unatokomezwa kabisa hapa nchini.

Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu athari yake ni kubwa katika jamii na ni kati ya magonjwa 10 yanayoongoza kupoteza maisha ya watu wengi ulimwenguni hasa katika nchi maskini ikiwemo Tanzania, hivyo jamii nayo inatakiwa kushiriki katika kuutokomeza ugonjwa huo hatari.

Dk Kihongole ambaye ni Mratibu wa tiba asili na mbadala alieleza kuwa taifa lenye watu wenye afya dhaifu kamwe haliwezi kupata maendeleo kwa sababu wananchi wake watatumia muda mwingi kujiuguza badala ya kushiriki kazi za kiuchumi.

Chanzo: habarileo.co.tz