Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahudumu wa afya watakiwa kumtanguliza Mungu

179dda61401cd2dbbb151fda9e726707 Wahudumu wa afya watakiwa kumtanguliza Mungu

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAHUDUMU wa afya nchini wametakiwa kufanya kazi yao ya kuokoa maisha ya wagonjwa kwa kumtanguliza Mungu kwanza kwani wamebeba dhamana ya maisha ya watu.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mchungaji, Rose Shaboka wa Kanisa la New Day wakati akizungumza na wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Taasisi hiyo.

Mchungaji Rose alisema wahudumu wa afya ni watu wa muhimu sana katika jamii na hata Biblia inawatambua kutokana na huduma ya matibabu wanayoitoa kwani Luka ambaye alikuwa mwanafunzi wa Yesu alikuwa ni tabibu.

“Dhamana ya uhai wa maisha ya watu mliyoibeba ni kubwa,kama mtakosea kumtibu mgonjwa na kumpa dozi isiyo sahihi atapoteza maisha fanyeni kazi yenu mkijua kuwa mnamtumikia Mungu ambaye atawalipa kutokana na huduma mnayoitoa.

“Kataeni kutumika kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili yenu ya kazi kama vile Farao alivyotaka kuwatumia wakunga kuwaua watoto wa kiume wa Israel wakati wanawazalisha wanawake wa Kiebrabia lakini wakunga hao walikataa na kufuata taratibu zao za kazi na hawakuwaua watoto wale,” alisema Mchungaji Rose.

Alisema amekuwa akifurahia kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo na kuwalipia gharama za matibabu kwani yeye ni mama na ana watoto ndiyo maana anasaidia watoto tangu mwaka 2020 alianza kutoa huduma hiyo.

Mtaalamu wa Afya ya Jamii kutoka Doctor's Plaza Polyclinic, Sophia Byanaku aliwapongeza wanawake hao wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kazi ngumu wanayoifanya ya kuokoa maisha ya watu.

Sophia alisema jambo la muhimu ni kuwaelimisha wanawake wanaotibiwa au kuuguza ndugu zao wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kutumia mitandao ya kijamii kufanya mambo yenye tija ambayo yatawaletea mafanikio katika familia zao.

Chanzo: www.habarileo.co.tz