Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Wahudumu wa afya jiongezeni’

30819 Afya+pic Mtaalamu wa magonjwa ya kinamama na uzazi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili

Mon, 10 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mtaalamu wa magonjwa ya kinamama na uzazi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas), Profesa Siriel Massawe amewataka wahudumu wa afya kuongeza ujuzi na juhudi katika kazi ili wananchi wapate huduma bora.

Profesa Massawe alitoa kauli hiyo jana katika siku ya pili kongamano la kujadili afya za wanawake wa jumuiya ya Afrika Mashariki lililowashirikisha wataalamu, watafiti, walimu wa afya na wadau wa maendeleo takribani 100 kutoka mataifa mbalimbali.

Kongamano hilo, liliandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kwa kushirikiana na Chuo cha Udaktari Bingwa cha Aga Khan tawi la Dar es Salaam, Muhas na Hospitali ya Aga Khan.

Profesa Massawe aliwataka wahudumu wa afya kushughulikia matatizo yanayowakabili wananchi hasa kina mama huku wakiwa na vitendea kazi bora vitakavyowasaidia katika majukumu yao.

“Aga Khan wamefanya jambo zuri sana (kuandaa kongamano), hata vyuo vingine vinajitahidi kufanya, Muhas huwa tunajitahidi kufanya mikutano ya namna hii kila mwaka,” alisema Profesa Massawe.

Mtaalamu wa Afya ya Jamii wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Dk Kahabi Isangula alisema uzoefu alioupata kutoka kwa wataalamu atahakikisha anausambaza kwa wahudumu wa afya hasa wa vijijini.

“Sehemu kubwa ya shughuli zangu nazifanya Shinyanga hasa vijijini. Nilichokipata hapa nitakwenda kushirikiana na wenzangu kupitia mradi wetu wa kuwajengea uwezo wahudumu wa afya vijijini ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Dk Isangula.



Chanzo: mwananchi.co.tz