Dar es Salaam. Serikali ipo mbioni kuanzisha mtihani wa kupima uwezo wa wahitimu wa fani zote za afya, zikiwemo muhimu za udaktari na uuguzi kabla ya kutoa leseni.
Lengo la mtihani huo ni kuhakikisha nchi inapata wataalamu bora wa afya na pia kuwahimiza kujiendeleza kitaaluma hata baada ya kuhitimu.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Bakari Kambi alipokuwa akifunga mkutano wa siku mbili wa kukusanya maoni ya wadau wa sekta ya afya, kuelekea kuanzishwa kwa mtaala linganifu wa mafunzo kwa watoa huduma za afya nchini, chini ya mradi wa THET.
Mkutano huo ulihusisha wadau kutoka vyuo vyote vya afya nchini, kutoka Tume ya Taifa ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Madaktari Tangayika (MCT).
Profesa Kambi, akizungumza kwa niaba ya katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Zainab Chaula alisema kuna sheria inayoelekeza kupima uwezo wa watahiniwa wa fani hiyo, akiitaja kuwa ni The Medical Dental and Allied Health Professionals Act namba 11 ya mwaka 2017.
Alisema sheria hiyo ilipitishwa mwaka juzi na ilisainiwa na Rais, inahitaji kanuni ziandaliwe, ikiwemo ya mtihani kwa wahitimu wa fani hiyo.
Alisema sheria hiyo inasema “mtu hawezi kusajiliwa chini ya sheria hadi akidhi vigezo”, kikiwamo cha kufaulu mtihani.
“Mtihani huu utafanyika mara baada ya kumaliza shahada. Kwa hivi sasa, kila chuo kina mtihani wake, lakini kupitia sheria hii Baraza litaandaa mtihani mmoja ambao utafanywa na wahitimu wote wa ndani na wa nje ya nchi,” alisema.
“Wahitimu kutoka vyuo vyote vya afya wataufanya ili kupima uwezo wao wa kutoa huduma za afya, ”alisema.
Alisema mtihani huo hautaishia kwa madaktari na wauguzi pekee, bali kwa kada zote bila ya kujali wametoka chuo gani.
“Moja ya mikakati yetu kama wizara ni kuhakikisha tunaboresha utoaji wa huduma za afya na ili uboreshe lazima wataalamu wapate vigezo,” alisema.