Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahitimu 181 kutunukiwa shahada za udaktari HKMU

359d665506f9d477fae6f73231c61005.jpeg Wahitimu 181 kutunukiwa shahada za udaktari HKMU

Fri, 11 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAHITIMU 181 wanatarajiwa kutunukiwa shahada za udaktari kwenye mahafali ya 18 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Profesa Hubert Kairuki (HKMU) kesho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chuo hicho jana, mahafali hayo yatafanyika chuoni hapo kuanzia asubuhi.

Taarifa hiyo ilisema kwenye mahafali hayo wahitimu wa shahada ya uuguzi watakuwa 53, wahitimu wa udaktari 181, wahitimu wa astashahada ya uuguzi 146 na mhitimu mmoja wa shahada ya magonjwa ya wanawake na uzazi.

Ilisema mhitimu mwingine mmoja atatunukiwa Shahada ya Uzamili ya Tiba na Afya ya Watoto na kwamba jumla ya wahitimu wote watakuwa 382.

“Makamu Mkuu wa HKMU, Profesa Charles Mgone anayo heshima kubwa kuutaarifu umma kuwa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki kitafanya mahafali ya 18 tarehe 12 Desemba 2020 kuanzia asubuhi,” aliongeza taarifa hiyo.

Aliwapongeza wahitimu hao kwa kumaliza masomo yao salama na kwa namna walivyoishi vizuri chuoni hapo.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Charles Mgone alisema hivi karibuni kuwa HKMU kimepanga kujitanua zaidi ikiwa ni jitihada za kuzalisha watumishi wa kada mbalimbali katika sekta ya afya ili kupunguza uhaba wa watumishi kwenye sekta hiyo.

Akizungumzia mikakati ya chuo hicho kuongeza udahili na kuzalisha madaktari na wakunga wengi zaidi, alisema kitahakikisha taaluma inazingatiwa katika kutoa madaktari na watumishi wengine wa kada ya afya.

“Sisi tuliona mbele kabisa kwamba katika sehemu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) tunaitumia kama msingi wa mafunzo ya vitendo, tunataka kila kitu kiwe kwenye elekroniki badala ya kutembea na makaratasi,” alisema.

Alisema chuo hicho licha ya kutoa madaktari wa shahada ya kwanza, pia kimekuwa kikifundisha na kuzalisha madaktari bingwa kwenye fani ya tiba.

Alisema kwa wastani kwa mwaka wamekuwa wakizalisha madaktari zaidi ya 200 na wanatarajia idadi hiyo itaongezeka kutokana na upanuzi wa chuo hicho unaotarajiwa kufanywa.

Chanzo: habarileo.co.tz