Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagonjwa wanaotibiwa BMH wongezeka

55671 Pic+wagonjwa

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Idadi ya wagonjwa wanaopata huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma (BMH) wameongezeka kutoka 50 hadi kufikia zaidi ya 200 kwa siku katika kipindi cha kati ya mwaka jana na mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha BMH, Meshack Karimu amesema hayo Jumamosi Mei 4 wakati waandishi wa habari walipotembelea hospitali hiyo kuona jinsi mkopo uliotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulivyonufaisha hospitali.

Amesema hospitali hiyo pia inatoa huduma za uchunguzi, matibabu, operesheni za figo na moyo.

Amesema wapo katika maandalizi makubwa ya kuanza matibabu ya uboho na kwamba ndio eneo kubwa  wanalolifanyia kazi kutokana na matibabu hayo kutopatikana nchini.

“Uwepo wa hospitali hii umepunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kwa asilimia kubwa. Ukizungumzia upandikizaji wa figo zamani tulikuwa tunapeleka wagonjwa nje ya nchi lakini sasa tunafanya hapa hapa nchini,” amesema.

Amesema tangu mwaka jana hospitali hiyo imeshapandikiza wagonjwa saba figo.

“Wagonjwa wameongezeka sana kati ya mwaka jana na mwaka huu. Miaka miwili ya mwanzo tulikuwa tunawaona wagonjwa 20 hadi 50 lakini katika kipindi cha mwaka jana na mwaka huu tunawaona wagonjwa kati ya 200 hadi 300 kwa siku,” amesema.

Amesema kuwa wagonjwa hao wanatoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Singida, Tabora, Morogoro Kilimanjaro, Kigoma, Manyara na Arusha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha NHIF, Angela Mziray amesema gharama za matibabu ni kubwa na ndio maana Serikali inahimiza watu kujiunga na mfuko huo ili waweze kuchangia kiasi kidogo kwa ajili ya kupata matibabu wanapohitaji.

“Kwa ujumla uwekezaji huu wa majengo na vifaa unathamani ya Sh 104 bilioni,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz