Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagonjwa wa dengue waongezeka D’Salaam

Fri, 17 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Idadi ya wagonjwa wa homa ya dengue katika Mkoa wa Dar es Salaam imeendelea kuongezeka na hadi jana wamefikia 1,809 kutoka 1,200 wa wiki iliyopita tangu ulipoingia nchini Januari.

Takwimu mpya zilizotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi jana, idadi ya watu waliopimwa na kuthibitika kuwa na ugonjwa huo ni 1,901 kati yao, 1,809 wakiwa Dar es Salaam.

Idadi hiyo ni ongezeko la wagonjwa 674 ikilinganishwa na takwimu zilizotolewa na Serikali Mei 10. Profesa Kambi alisema ongezeko hilo ni wastani wa wagonjwa 75 kwa siku ikiwa ni tofauti na wastani wa wagonjwa 32 waliopatikana Aprili.

Kata ya Ilala ndiyo inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi ambao idadi yake imefikia 235 ikifuatiwa na Sinza yenye wagonjwa 223.

Mkoa wa unaoshika nafasi ya pili ni Tanga wenye wagonjwa 89 huku Singida, Pwani na Kilimanjaro ikiwa na mgonjwa mmoja mmoja ambao baada ya kufanyiwa uchunguzi ilibainika kuwa wote walitokea Dar es Salaam.

Profesa Kambi alisema idadi hiyo inaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha watu wanapata elimu na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Pia Soma

Alisema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ikiwamo kutoa elimu, kuhamasisha usafi wa mazingira kuondoa mazalia ya mbu pamoja na kuhimiza wagonjwa kuwahi hospitali.

Kwa upande wa matibabu, Profesa Kambi alisema Serikali imehakikisha hospitali na vituo vyake vya afya sasa vimefikia 19 vinakuwa na uwezo wa kupima ugonjwa.

Pia, alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuongeza idadi ya vitendanishi kwenye vituo hivyo huku vingine vikiendelea kuagizwa kutoka nje ya nchi. “Tumeagiza test kits 3,000 ambazo zina uwezo wa kupima watu 30,000. Kati ya hivi 200 ziko tayari na tutavisambaza kwenye hospitali za Dar na zingine zitakuja,” alisema.

Sanjari na hilo alisema wizara inaandaa mpango wa dharura kukabiliana na ugonjwa huo unaokwenda sambamba na kupelekea timu maalumu Dar kusaidiana na wataalamu waliopo.

Aliwasihi Watanzania kuachana na taarifa za mitandaoni kuhusu uwepo wa tiba ya ugonjwa huo na badala yake kusikiliza maelekezo yanayotolewa na Serikali.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yudas Ndugile alisema jitihada zinaendelea kuchukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kunyunyuzia viuatilifu katika maeneo yenye mazalia ya mbu na kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi kwenye kata zilizoathiriwa zaidi zikiwzmo za Ilala, Sinza na Upanga.

Pia alisema mkakati mwingine ni kuwahimiza wananchi kujikinga dhidi ya mbu waenezao ugonjwa huo pamoja na kusafisha mazingira.

Pamoja na hatua hizo, Dk Ndugile alieleza kuwa kwa sasa mkoa upo kwenye mpango wa kuangamiza mbu kwa kuwapulizia dawa maalumu.

Chanzo: mwananchi.co.tz