Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagonjwa 55,000 wadaiwa kueneza TB

90b40381d8d602f0a83129a2b8f92a49 Wagonjwa 55,000 wadaiwa kueneza TB

Sun, 28 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAGONJWA 55,000 wa kifua kikuu (TB) nchini wanadaiwa kueneza ugonjwa huo katika jamii kutokana na wao kutorudi tena hospitali kupata tiba baada ya kugunduliwa kuwa na maabmukizi ya ugonjwa huo.

Mratibu wa Mpango wa Taifa wa TB na Ukoma kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Allan Tarimo alisema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO mwishoni mwa wiki na kusema wagonjwa wengine 82,000 waliogundulika wako kwenye tiba.

Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zinazoadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani Machi 24 kila mwaka.

Dk Tarimo alisema nchini Tanzania kwa mwaka 2019 ilikadiriwa kuwa na wagonjwa wa TB takribani 137,000 na kati ya hao waliwagundua na kuwaweka kwenye tiba ni wagonjwa 82,000 ambao ni sawa na asilimia 53 tu.

"Hii ina maana hatukuweza kuwapata wagonjwa 55,000 ambao wameendelea kueneza ugonjwa huu katika jamii yetu. Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ukiongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa, takribani asilimia 20 ya wagonjwa wote nchini walipatikana Dar es Salaam. Mikoa ya Kigoma, Songwe, Katavi na Zanzibar kwa ujumla imekuwa na idadi ndogo ya wagonjwa," alisema.

Alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye idadi kubwa ya maambukizo ya TB.

Alisema kidunia nchi ya India ndio inaongoza kwa kuwa na wagonjwa takribani milioni mbili kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu za WHO za mwaka 2019.

Alitaja makundi yanayoathirika zaidi na ugonjwa huo kuwa ni ambayo kinga ya mwili ni dhaifu na pia wale wanaofanya shughuli au kazi zinazosaabisha mtu kuugua kwa urahisi.

Alisema wizara imebainisha makundi ambayo yapo kwenye hatari ya kuambukizwa kuwa ni watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wenye utapiamlo, wachimbaji wadogo wa madini, na wanaojidunga dawa za kulevya.

Wengine ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 60, wagonjwa wa kisukari na magonjwa ya saratani, wafungwa, mahabusu, wanaoishi katika mabweni na watoa huduma za afya.

Alisema serikali inajitahidi kupambana na ugonjwa huo kwa kuboresha na kuongeza wigo wa huduma za ugunduzi wa TB kwa kutumia teknolojia ya vinasaba ya Gene-Xpert.

Dk Tarimo alisema wizara pia imeongeza mashine za GeneXpert zinazopima TB kutoka mashine 65 mwaka 2015 hadi 259 kwa mwaka 2020.

Chanzo: www.habarileo.co.tz