Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagonjwa 5000 kutoka nje wanakuja kutibiwa nchini kila mwaka

Wagonjwa 5000 Kutoka Nje Wanakuja Kutibiwa Nchini Kila Mwaka Wagonjwa 5000 kutoka nje wanakuja kutibiwa nchini kila mwaka

Thu, 4 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, zaidi ya Wagonjwa 5000 kutoka nje ya nchi zinazoizunguka Tanzania huja kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kila mwaka kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika eneo la miundombinu, vifaa tiba na watumishi wenye ujuzi mkubwa.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Mei 03, 2023 alipofanya ziara na kuongea na Watumishi wa afya katika Hospitali ya kanda ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

Amesema “Watu wanaotoka nje ya nchi zinazotuzunguka kwa mwaka kuja kupata huduma za kibingwa na kibingwa bobezi ni zaidi ya 5000, kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Rais Samia katika Sekta ya Afya. ” Amesema Dkt. Mollel.

Ameendelea kusema kuwa, tayari Serikali ya Tanzania imesaini mikataba na nchi za Zambia, Malawi kwaajili ya kuleta wagonjwa wao nchini kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imepunguza 97% ya wagonjwa kwenda kupata matibabu nje ya nchi, kutokana na uwekezaji wa vifaa tiba, miundombinu pamoja na watumishi wenye ujuzi, hivyo kuifanya nchi ya Tanzania kuwa kimbilio la matibabu kwa baadhi ya nchi ikiwemo nchi zilizo majirani na Tanzania.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Rais Dkt. Samia tayari ametoa zaidi ya Bilioni 51.4 katika hospitali za kanda ndani ya mwaka huu katika eneo la ujenzi, huku zaidi ya Bilioni 290.9 zimetumika kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye hospitali za Rufaa za Mikoa, Kanda na taifa.

Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema, pamoja na Mhe.Rais kufanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Afya kwenye maeneo yote ikiwemo miundombinu, vifaa tiba na watumishi wenye ujuzi, ipo haja ya kusimamia ubora wa huduma ili wananchi wanufaike katika maeneo mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live