Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagonjwa 12 watibiwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo

F194bc6758d195da6246c53829ad430c.jpeg Wagonjwa 12 watibiwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo

Mon, 13 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wagonjwa 12 ambao mfumo wa wa umeme wa moyo ulikuwa na hitilafu na kusababisha mapigo ya moyo kupiga bila mpangilio wamefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo wa kurekebisha hitilafu hiyo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo iliyomalizika hivi karibuni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Yona Gandye alisema kambi hiyo ilikuwa mahususi kwa ajili ya kutoa tiba kwa wagonjwa wenye matatizo ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi.

Dkt. Gandye alisema wagonjwa wanne (4) kati ya wagonjwa 12 waliofanyiwa upasuaji huo wamepata tiba ambayo imefuta kabisa tatizo la hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na sasa wapo kwenye mfumo wao halisi wa mapigo ya moyo hivyo basi baada ya miezi mitatu dawa walizokuwa wanazitumia wanaweza kuziacha na kutozitumia kabisa.

“Wagonjwa nane ambao walikuwa na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo ujulikanao kwa jina la kitaalamu kama “atrial fibrillation”ambao hufanya moyo kwenda haraka na mapigo ya moyo kutokuwa na utaratibu maalum wataendelea kufuatiliwa kupita kliniki zao ili kuhakikisha wanarejea katika hali zao za kawaida”,.

“Aina hii ya ugonjwa mara nyingi huweza kugandisha damu kwenye chemba ya “atrium” hivyo kusababisha kiharusi kitakachomfanya mgonjwa kupooza upande mmoja wa mwili ama kupoteza uhai”, alisema Dkt. Gandye.

Akizungumzia kuhusu matibabu hayo Dk. Gandye alisema upasuaji huo mdogo umefanyika kupita mtambo wa kisasa wa carto 3 unaoweza kuchora katuni ya moyo unavyoonekana kwa wakati huo na kuwasaidia wataalam kufika kwenye sehemu husika inayozalisha mapigo ya moyo ambayo yanaleta hitilafu, kufanya utaratibu wa mapigo ya moyo kuvurugika na kuwawezesha kurekebisha umeme huo kwa ufanisi.

“Kambi hii ilikua ya kubadilishana ujuzi baina ya madaktari wa JKCI na wenzetu mabingwa kutoka Misri ikiwa ni sehemu ya kutengeneza mahusiano na kujifunza mbinu mbalimbali za kitabibu katika kutoa huduma za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo”, alisema Dkt. Gandye

Aidha Dkt. Gandye alisema kwa kuwa hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo inaweza kutokea na mtu asiwe na dalili, ifike wakati jamii iwe na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya kila baada ya mwezi ama miezi mitatu, hii iitawasaidia wataalamu kubaini wale ambao hawana dalili lakini wana tatizo kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza madhara ya kutanuka kwa moyo, ama moyo kushindwa kufanya kazi hivyo kusababisha vifo vya ghafla.

Kwa upande wake mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mdogo wa kurekebisha mfumo wa umeme wa moyo Magesa Nyamhanga amewapongeza wataalam wa JKCI kwa kutoa huduma za kibingwa za matibabu hayo kwani hakutarajia kama huduma hiyo angeweza kuipata hapa nchini.

“Ninafuraha kuwa upasuaji wangu ulienda vizuri, taasisi hii imewekeza sana katika taaluma na vifaa vya kisasa, nimepata huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali lakini kusema ukweli hospitali zote nilizopita hakuna itakayoifikia JKCI”,.

“Tatizo la mfumo wangu wa umeme wa moyo nilizaliwa nalo lakini halikuwa likinisumbua sana, ilipofika mwaka 2020 tatizo hili lilianza kunisumbua na kuanza kutumia dawa sasa nimefanyiwa upasuaji wa kurekebisha mfumo wa umeme wa moyo na mabadiliko ya mapigo yangu ya moyo baada ya upasuaji nayasikia yako tofauti”, alisema Magesa.

Magesa aliiomba Serikali kuendelea kuongeza wataalam wa tiba ya mfumo wa umeme wa moyo nchini ili kusaidia wagonjwa wenye tatizo hilo kupata matibabu kirahisi kwani tatizo lipo na kama halitapatiwa matibabu kwa wakati watu wanaweza kupoteza maisha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz