Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi elimu ya juu wataka mambo 6 corona

THTU ED.webp Wafanyakazi elimu ya juu wataka mambo 6 corona

Sat, 25 Apr 2020 Chanzo: --

CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu za Juu Tanzania(THTU), kimetoa mapendekezo sita ya namna ya kukabiliana na athari zinazotokana na janga la corona hususan kwenye sekta ya elimu.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni vyuo vikuu, taasisi za elimu ya juu na vyuo vya kati kutumia fursa za Tehama kuendelea na masomo yanayowezekana kwa njia ya mtandao ili kusaidia kupangilia vizuri mihula ya masomo.

Pia, kinapendekeza serikali irasimishe utaratibu wa utoaji wa elimu kupitia mitandao na vyombo vya habari ikiwamo redio na televisheni hasa wakati huu wa corona.

Akitoa mapendekezo hayo mbele ya waandishi wa habari jijini hapa jana, Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk. Paul Loisulie, alisema ugonjwa wa corona umeleta athari katika sekta ya elimu na wanaona ni wakati sasa kwa vyuo na taasisi hizo kunusuru hali hiyo badala ya kusubiri hadi ugonjwa huo uishe.

Alisema pamoja na jitihada za kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo, tayari athari zimeshaonekana na nyingine zitaonekana siku zijazo.

“Hatupaswi kuendelea kusimama katika taratibu za kawaida tulizozoea wakati corona imeshavuruga taratibu, ni lazima tujipange na kutafuta utaratibu mbadala wa kukabiliana na athari za sasa na zijazo,” alisema.

Alisema THTU inashauri vyuo vionyeshe umahiri wao wa kutumia fursa za Tehama kuhakikisha vipindi vinaendelea kwa yale masomo yanayowezekana kwa njia ya mtandao.

“Hii ni njia mbadala ambayo itasaidia taasisi hizi kupangilia vizuri mihula ya masomo pale ugonjwa huu utakapodhibitiwa na kukaa kusubiri tatizo liishe ndipo kuchukua hatua ni kutojitendea haki wenyewe, kutoitendea haki jamii na nchi kwa ujumla,” alisema.

Alitoa wito kwa serikali kuwezesha taasisi hizo kufanikisha malengo hayo na kutoa msaada kwa taasisi za binafsi ambazo kwa wakati huu zinapitia wakati mgumu kufuatia vyanzo vyao vikubwa vya mapato kusimama kutokana na wanafunzi wengi kutolipa ada kwa wakati huu.

Dk. Loisulie alisema utaratibu ulioanzishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wa utoaji wa elimu mtandaoni na kwenye televisheni, uboreshwe zaidi kwa kuhusisha redio ili kuwafikia wanafunzi wote nchi nzima.

“Ili kutoharibu mtiririko wa mihula, wanaweza wakatafutwa walimu wa kila somo na kurekodi vipindi (mada zote) ambazo zitarushwa kwenye redio zote nchi nzima na wanafunzi kutakiwa kusikiliza na kufanya majaribio,” alisema.

Mwenyekiti huyo alishauri kampuni za simu zilizopo nchini kutafuta namna ya kupunguza gharama za vifurushi vyao vya intaneti na pia miamala yao wakati huu wa corona ili watu wengi wafanye malipo kwa kutumia mitandao ya simu bila kuhofia gharama.

“Fedha ambayo huwa inatumika kutimiza azma ya wajibu kwa jamii inaweza kusaidia kutumika kwa njia hii ya kupunguza gharama za miamala na vifurushi,” alishauri.

Dk. Loisulie pia alishauri wizara zote zijielekeze katika kutengeneza taratibu na mazingira wezeshi yatakayoendelea kulinda mazingira ya kiuchumi na kijamii kwa mwananchi wa kawaida na pia kulinda shughuli za kiuchumi za biashara mbalimbali ili kulinda ajira za wafanyakazi wengi.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo alisema taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu zinapaswa kuchukua hatua ya kufanya utafiti na machapisho juu ya ugonjwa huo badala ya kusubiri machapisho na utafiti kutoka vyuo vya Ulaya na Marekani.

Pia, alisema ni wakati mwafaka wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa kutekeleza dhana ya Tanzania ya viwanda kwa kutengeneza bidhaa zitakazouzwa ndani na nje ya nchi ili kuondoa upungufu wa bidhaa na huduma zilizokuwa zinaletwa kutoka nje ya Tanzania kabla ya janga hilo.

Chanzo: --