Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafamasia hawa wapewa siku 14 kujisalimisha

C235c7aa2f4c4ab9a8f9f6fb8b38e900 Wafamasia hawa wapewa siku 14 kujisalimisha

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MSAJILI wa Baraza la Wafamasia nchini, Elizabeth Shekalaghe ametoa siku 14 kwa wafamasia wanaosimamia maduka ya dawa lakini hawapo katika maeneo yao ya kazi kujisalimisha katika baraza hilo.

Shekalaghe alitoa agizo hilo jijini Dodoma jana, akisisitiza kuwa wafamasia wanaosimamia maduka ya dawa lakini hawapo ndani ya maeneo yao ya kazi kuanzia jana wajisalimishe katika baraza hilo.

“Mtu anakaa Morogoro anasimamia duka la dawa Dodoma lakini taarifa alizotuletea sisi yupo Dodoma, sasa tumeshaanza kufanya ufuatiliaji maalumu ili kuwabaini."

"Kifungu Na. 43 cha Sheria ya Famasi, Sura 311 kinaelekeza kwamba, hairuhusiwi mtu yeyote kujihusisha na biashara ya famasi kama sio mfamasia, endapo mtu huyo atahitaji kufanya hivyo atalazimika kutafuta mfamasia ili asimamie huduma hiyo," alisema.

Shekalaghe alisema pia kanuni ya 10 ya Kanuni za Utendaji wa Taaluma za Mwaka 2020 inaelekeza kwamba mfamasia atawajibika na usimamizi wa huduma katika duka hilo la dawa kila siku.

“Kwa kiasi kikubwa bado wafamasia wengi hawawajibiki kwa kiwango cha kuridhisha katika maeneo yao ya kutolea huduma, alisema.

Alisema hivi karibuni kumekuwa na tabia ya wafamasia kuingia mikataba na wamiliki wa maduka ya dawa huku wakishindwa kutekeleza majukumu yao, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za utendaji wa taaluma hiyo.

“Ni kosa kwa mfamasia kutokufika katika eneo la kazi. Kanuni ya 13 ya Kanuni za Usajili wa Famasi inaelezea kuwa, kutofika kwa mfamasia katika famasi anayofanyia kazi ni moja ya sababu za kufutwa kwa kibali cha uendeshaji wa huduma hizo kwa sababu ya kukosa usimamizi,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz