Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waandishi wafundwa kuhusu afya ya uzazi

Fri, 5 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waandishi wa habari wanawake Tanzania wameanza kunolewa kuhusu afya ya uzazi baada ya kuonekana muda mwingi wanatumia kuhudumia jamii na kusahau masuala yanayohusu afya zao binafsi.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Alakoki Mayombo amesema badala ya kuripoti peke yake wanawake wanahabari wanatakiwa kuchukua hatua kwa kujua afya zao binafsi.

Akifungua mafunzo hayo siku moja leo Ijumaa Aprili 5, 2019 kabla ya mkutano mkuu wa Tamwa, Mayombo amesema katika vikao vyao waligundua kuna haja kwa waandishi wa kike kupewa mafunzo hayo.

Amesema mafunzo hayo yanatolewa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Narayana iliyopo nchini India.

"Baada ya mafunzo watakutana na madaktari na kupewa ushauri kuhusu afya zao, tunafanya hivi ili hata wanapoandika wawe wanajua afya zao," amesema.

Awali, Mkurugenzi wa Tamwa, Rose Reuben amesema mbali na elimu ya afya wanahabari hao watanolewa kuhusu masuala ya mitandao.

Amesema ujio wa mitandao ya kijamii umeongeza fursa kwa taaluma hiyo hivyo waliona umuhimu wa kuwafundisha namna ya kutumia wakifuata kanuni na sheria zilizopo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz