Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema linaunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kuanzisha Mfuko wa Pamoja wa Bima ya Afya.
WHO inaunga mkono juhudi hizo wakati Serikali ya Tanzania ikiwa kwenye mpango wa kuunganisha Mfuko wa Afya ya Jamii na Bima ya Afya ili kuwezesha wananchi wote kupata huduma bora za afya.
Akizungumza leo Jumatano Juni 26, 2019 Mtaalamu wa Uchumi wa WHO nchini Tanzania Maximilian Mapunda amesema jambo la msingi ni kila mtu kupata huduma bora za afya bila kujali uwezo wake kifedha.
Mapunda amesema malipo ya matibabu kabla ya kuugua yanamsaidia mtu kuhudumiwa bila kipingamizi jambo wanalotilia mkazo zaidi.
"WHO tunatilia mkazo utoaji wa huduma za afya kwa wote bila kuwepo kikwazo cha fedha kwa hiyo mfuko wa pamoja wa bima za afya ni jitihada tunazounga mkono," amesema Mapunda.
Awali, baadhi ya wajumbe wa mkutano wa huduma za afya kwa wote 'Health Universal Coverage' wamesema sekta binafsi inao mchango mkubwa katika kuhudumia afya ya jamii hivyo haipaswi kuwekwa pembeni katika mikakati ya utoaji huduma hizo.
Pia Soma
- Tuhuma za rushwa ya Sh700,000 zamfikisha kortini Askari JWTZ
- Mahakama yafungua huduma ya intaneti kwa raia mmoja tu nchini Sudan
- TFS yajitosa kusaidia sekta ya elimu Mbeya