Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WHO yatoa tathimni ugonjwa wa TB

Kifua Kikuu.jpeg WHO yatoa tathimni ugonjwa wa TB

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la Afya duniani (WHO) limesema idadi ya vifo vya kifua kikuu (TB) imeongezeka katika kipindi cha 2021.

WHO imetaja mambo yaliyochangia kuwa ni pamoja na kupungua kwa upatikanaji wa huduma za upimaji na matibabu ya ugonjwa huo, kutokana na janga la Uviko-19.

Hayo yamesemwa jana Jumatano Machi 23, 2022 na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Shirika la Afya Ulimwenguni, Dk Matshidiso Moeti alipokuwa akitoa tamko la siku ya TB duniani inayotarajiwa kuadhimishwa kesho kwa kauli mbiu “Wekeza kukomesha TB. Okoa maisha” inayosisitiza haja ya dharura ya kuwekeza rasilimali zinazohitajika ili kuimarisha mapambano dhidi ya TB.

Dk Moeti amesema ili kufikia shabaha za malengo endelevu lazima kuwe na uwekezaji kuhakikisha kuwa huduma za kifua kikuu TB zinaunganishwa katika huduma ya afya ya msingi

“Ili kufikia shabaha za malengo endelevu visa vya kifua kikuu vilipaswa kupungua kwa mwaka kwa asilimia 4 hadi 5 kwa mwaka 2020, kuongezeka hadi asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2025 na kisha hadi wastani wa asilimia 17 kila mwaka katika muongo uliofuata, lakini tumeshuhudia vifo vikiongezeka mwaka 2021,” amesema.

Amesema kwa kuwa asilimia 36 ya vifo vyote vya TB vinatokea barani Afrika, kushindwa kuwekeza katika mwitikio wa ugonjwa huo kunatarajiwa kuleta athari mbaya kwa nchi za Kiafrika.

Kwa upande wa Tanzania, takwimu mpya zinaonyesha jumla ya watu 87,000 wamegundulika na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na wengine 26,800 wamefariki dunia.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema, “Kuna changamoto kubwa ya kuwabaini wagonjwa wapya. Mwaka jana tuligundua wagonjwa wapya 87,000 na makadirio tuna wagonjwa wapya 133,000 kila mwaka lakini tunaweza kuwabaini asilimia 66 ndiyo inayofikiwa na kwa upande wa vifo vilikuwa 26,800.”

Katika mkutano wa ngazi ya juu wa umoja wa mataifa kuhusu TB mwaka 2018, viongozi wa dunia walikubaliana kukusanya dola za Marekani bilioni 13 kwa mwaka ili kufadhili kinga na matibabu ya TB ifikapo mwaka 2022 na kuahidi dola bilioni 2 kwa mwaka kwa ajili ya utafiti wa TB katika kukabiliana na kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu kifua kikuu sugu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live