Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WHO yatoa angalizo la bima ya afya

Whopic Data WHO yatoa angalizo la bima ya afya

Sun, 12 Dec 2021 Chanzo: Mwananchi

Imeelezwa kuwa uwepo wa mifuko mingi ya bima ya afya italeta mkanganyiko katika utoaji wa huduma hiyo.

Akizungumza na vyombo vya habari jana, Ofisa mtaalamu wa uchumi wa afya kutoka WHO, Maximilian Mapunda alisema mfumo uliopo nchini ni wafanyakazi ndiyo wenye uwezekano wa kuchangia, lakini mfumo wa kodi unaonekana ndiyo mzuri zaidi kufikia afya kwa wote.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alipoulizwa kuhusu ushauri huo alisema: “Mpango huo upo, kwa sasa unaandaliwa muswada wa sheria ya uanzishwaji wa bima ya afya kwa wote bungeni.”

Mapunda alisema nchi nyingine huamua kuanzisha mifuko ya afya hivyo kama utaanzishwa uwe mmoja kusiwe na mifuko mingi.

“Ikiwa mingi ni risk kwenye ile mifuko hutaweza kuhakikisha wenye mahitaji wanapata huduma, nchi zilizofanya vizuri kwenye mradi huo ziliamua kutumia mfuko mmoja,” alisema.

Advertisement Alisema maamuzi hayo yatasaidia kwani walio katika mfumo usio rasmi kuna wakati wana mapato ya muda wanaweza wakachangia. “Tafiti nane zimefanyika na washauri wa kitaalamu wamependekeza kuandaa utaratibu wa mfuko mmoja.”

Mkurugenzi Mkaazi wa WHO Tanzania, Dk Tigest Ketsela Mengestu alisema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, magonjwa ya kuambukiza ni mzigo mkubwa, hivyo uwezekano wa kuwepo mpango wa afya kwa wote utasaidia idadi kubwa ya Watanzania ambao wamekuwa wakiingia kwenye umaskini kutokana na kulipia huduma za afya.

“Afya kwa wote ni stahiki ya kila mtu, bila kujali vipato vyao ni vya aina gani, muhimu ni kuhakikisha wanapata huduma za afya pale wanapohitaji, mwaka 2010 WHO ilikuwa na mpango huu na umewekwa katika lengo namba 3 la malengo endelevu ya dunia,” alisema.

Hata hivyo madaktari wameeleza wasiwasi wao kuhusu matumizi ya bima moja na huduma kuwa sawa kwa watu wote.

Rais wa Chama cha Madaktari, Shadrack Mwaibambe alisema katika uboreshaji wa huduma za afya kinachoangaliwa ni upatikanaji wa huduma, zilizopo muda wote na katika gharama ambayo mtu ataimudu na endelevu.

Alisema changamoto kubwa ni kwenye gharama, kwani wengi hawawezi kumudu, mpaka mwaka 2020 ni asilimia 17 pekee ya Watanzania ambao walikuwa wameunganishwa na bima ya afya. “Unaweza ukaona asilimia 83 ya Watanzania hawajafikiwa na huduma na kiuhalisia watu wanaoweza kulipia matibabu kwa fedha kutoka mfukoni ni wachache, hasa wanapougua.

“Serikali ikiongeza bajeti kwenye dawa zinaenda ngazi za chini huko ambako kuna gharama nafuu, lakini bado hawawezi kumudu, hawajitokezi kutibiwa na wakijitokeza ugonjwa umezidi sana, wengine wanaenda wakiwa na hali mbaya na wengine wanaenda tiba asili,” alisema.

Mwaibambe alisema afya kwa wote ni huduma nzuri, tatizo ni gharama ingawaje nchi haijawahi kujaribu lakini mfumo huo ukiwepo nchini utasaidia, ijapokuwa ni ngumu sana watu wote wakawa na uwiano sawa wa maisha.

“Huwezi kuwaweka matajiri na maskini katika huduma sawa za kiafya, ndiyo maana unasikia malalamiko kwamba hospitali fulani wana gharama kubwa mtu mwenye fedha aende. Sababu hatujawahi kuingia huko ngoja tujaribu, tunaunga mkono lakini kama mimi binafsi hatuwezi kupata huduma sawa bado hatujafikia huko,” alisema.

Mwaibambe alifafanua zaidi kwa kusema kuna mkanganyiko na ndiyo maana hata mifuko ya pensheni ilitengwa miwili yaani NSSF na PSSSF.

“Walifanya hivyo kwa sababu huu mfuko wa bima ya pamoja nina wasiwasi unaweza kuleta huduma za ajabu baadaye, lakini mimi bado nina maswali mengi kuhusu hilo, si kila waliofanikiwa walianza mara moja wakafanikiwa.”

Suala la mchakato wa bima ya afya kwa wote limekuwa likisuasua kiasi cha Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kuamua kulivalia njuga.

Akiahirisha Bunge Novemba 2, Spika Ndugai alimuita Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ambaye wakati huo hakuwepo ndani ya ukumbi wa Bunge akisema waziri amepiga tikitaka kubwa.

Ndugai alisema chenga za Serikali katika jambo la bima ya afya kwa wote zimekuwa nyingi na ziliwashinda wabunge kwa miaka mitano 2015/20 ambayo kati ya mikutano 19 na 20 walikuwa wakikumbushia lakini halikufanikiwa.

Kwa mujibu wa Ndugai, kama Bunge hili Serikali imeshindwa kupeleka muswada bungeni, ina maana mategemeo ya kupata ni Novemba 2022 ambao utakuwa ni mkutano wa tisa katika uhai wa Bunge la 12.

Hivyo, Spika alimwagiza Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya huduma za Jamii, Stanslaus Nyongo aanze kuisumbua wizara kwa kuwa akikaa kimya, atafeli kama walivyofeli wenzake waliomtangulia na kuagiza wabunge wanawake wasimamie kwa nguvu jambo hilo.

Ndugai alisema kwa sasa wanaidai bima ya afya kwa sababu ndiyo kipaumbele namba moja kwa wananchi, ajenda za maendeleo ni mengineyo, kwa hiyo lazima itungwe sheria ya bima ya afya kwa wote wananchi waanze kunufaika.

Virusi vya Omicron

Wakati virusi vya Omicron vikizidi kusambaa nchi mbalimbali, Watanzania wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata miongozo yote ya kujikinga na Uviko-19, ikiwemo kuchanja kwa kuwa bado hakuna taarifa za kutosha kuhusu kirusi hicho.

Kirusi hicho kinachoitwa B.1.1.529 tayari kuna mamia ya visa vimethibitishwa katika jimbo la Gauteng (Afrika Kusini) na Botswana, Hong Kong, India na nchi nyingine ambapo vimehusishwa moja kwa moja na watu kusafiri wakitokea Afrika Kusini.

Mkurugenzi Mkaazi wa WHO Tanzania, Dk Tigest Ketsela Mengestu alisema: “Katika wimbi hili bado kuna maswali mengi ambayo WHO inajiuliza na itachukua wiki kadhaa kukamilisha utafiti juu ya Omicron na kuona ikiwa kuna mabadiliko yoyote katika maambukizi, ukali au athari katika chanjo za Uviko-19, vipimo na matibabu yake. Kwa hiyo taarifa itatolewa pindi yakipatikana majibu kuhusu kirusi hicho.”

Dk Mengestu aliwataka wananchi kuchukua tahadhari zote, ikiwamo kuchanja ili kujiweka imara zaidi na kirusi hicho, lakini pia virusi ambavyo vilikuwepo tangu awali.

“Hiki ni kipindi ambacho watu wanakwenda kukusanyika, hivyo tusisahau kwamba kuna Uviko-19, tuhakikishe tunachukua tahadhari zote ili kuhakikisha tunakuwa salama,” alisema.

Ofisa anayehusika na masuala ya majanga na dharura Dk Grace Saguti alizungumzia taarifa za baadhi ya nchi kuwekewa vikwazo kutokana na ugonjwa huu.

Chanzo: Mwananchi