Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WHO yatangaza homa ya nyani mlipuko wa dunia

Monkey Poxyyyy WHO yatangaza homa ya nyani mlipuko wa dunia

Sun, 24 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ugonjwa wa homa ya nyani maarufu ‘monkey pox’ umetangazwa rasmi kuwa janga la dunia baada ya kuathiri zaidi ya watu 16,000 katika nchi 75.

Mei 19, 2022 mwathirika wa virusi vya monkey pox aliripotiwa nchini Uingereza baada ya mtu ambaye alikuwa amesafiri kutokea nchini Nigeria kugundulika kuwa na virusi hivyo nchini humo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus wakati akitangaza dharura hiyo mbele ya vyombo vya habari jijini Geneva, Uswisi.

Mlipuko huo uliotajwa kusababisha vifo vitano barani Afrika, umetangazwa baada ya timu ya wataalamu kupambana nao kwa takribani miezi kadhaa.

Tahadhari iliyotolewa ni ya juu kabisa inayoweza kutolewa na Shirika la WHO kuhusu dharura yoyote ya kiafya duniani.

“Kwa mwaka huu walioathirika na ugonjwa huo ni 16,000 katika nchi zaidi ya 75 na vifo vitano barani Afrika,” amesema Dk Tedros.

Amesema tathmini ya WHO inaonesha kiwango cha kusambaa kwa homa hiyo duniani bado ni cha wastani isipokuwa barani Ulaya ambako maambukizi yanaongezeka, Marekani imetajwa kuongezeka kwa maambuki hayo huku asilimia 98 ya walioambukizwa wakiwa ni wanaume.

“Ulaya kwa sasa ndiyo kitovu cha mlipuko huo, ikiripoti zaidi ya asilimia 80 ya maambukizi yaliyothibitishwa duniani kote mwaka wa 2022. Marekani imeripoti zaidi ya waathirika 2,500 vya homa hiyo hadi sasa katika majimbo 44, Washington D.C na Puerto Rico,” amesema Dk Tedros.

Kuhusu homa ya nyani

Ugonjwa huo husababishwa na virusi vya monkey pox, kirusi wa familia moja ya virusi vya ndui, ingawa sio kali sana na wataalamu wanasema uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo.

Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo, kuuma kwa misuli na udhaifu wa mwili kwa ujumla.

Mara baada ya homa, upele unaweza kutokea, mara nyingi huanza kwenye uso, kisha kuenea kwa sehemu nyingine za mwili, kwa kawaida viganja vya mikono na nyayo za miguu.

Upele, ambao unaweza kuwasha sana ambao hutengeneza kipele, ambacho hutumbuka baadaye. Vidonda vinaweza kusababisha makovu.

Maambukizi kawaida huisha yenyewe na hudumu kati ya siku 14 na 21.

Monkey pox inaweza kuambukizwa wakati mtu yuko karibu na mtu aliyeambukizwa. Virusi vinaweza kuingia mwilini kupitia ngozi iliyo na jeraha au michubuko, kwa njia ya upumuaji au kupitia macho, pua au mdomo.

Inaweza pia kuenezwa kwa kugusana na wanyama walioambukizwa kama vile nyani, panya na kindi au kwa vitu kama vile mashuka, mablanketi na nguo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live