Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WHO kuhusu wazazi wenye Corona kunyonyesha watoto

Nyonyo Ed Unyonyeshaji

Wed, 4 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

Uchunguzi wa Nipashe kupitia vyanzo vya kimataifa, likiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), umehakikishiwa hakuna uhusiano kati ya unyonyeshaji maziwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na maambukizi ya corona.

Akizungumza na Nipashe jana, Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo na Elimu Lishe kutoka TFNC, Dk. Ester Nkuba, alisema: “Maziwa ya mama mwenye ugonjwa wa virusi vya corona ni salama kwa mtoto wake, anashauriwa kuendelea kunyonyesha kwa kuzingatia tahadhari za kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa majisafi tiririka na sabuni na kukaa karantini wakati akiendelea kunyonyesha."

Mtaalamu huyo alikumbusha mama anayenyonyesha anapaswa kuzingatia mlo kamili na kwa wakati, unaojumuisha makundi matano muhimu ya lishe.

Dk. Ester alitaja sehemu ya mlo huo unajumuisha maji, matunda, mboga za majani, nafaka, mizizi, mafuta na nyama.

WHO katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu, Dk.Tedros Adhanom, inaeleza kuwa kinamama wanatakiwa kuhakikisha unyonyeshaji unaendelea kwa sababu ni salama kwa mtoto.

Dk. Adhanom anasema ni uzushi kuwa kunyonyesha kunaweza kusambaza virusi vya corona kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na badala yake wananchi waendelee kuhimiza unyonyeshaji watoto.

“Katika nchi nyingi, janga hili limesababisha usumbufu mkubwa katika huduma za msaada wa kunyonyesha, huku likiongeza hatari ya ukosefu wa chakula na utapiamlo.

“Nchi kadhaa zimeripoti kuwa wazalishaji wa vyakula vya watoto wameongeza hatari hizi kwa kutumia hofu isiyo na msingi kwamba kunyonyesha kunaweza kusambaza ugonjwa wa corona na kutangaza bidhaa zao kama njia mbadala salama ya kunyonyesha,” alisema mkuu huyo wa WHO.

Aliwakumbusha waajiri wa kampuni kutenga maeneo rasmi ya kunyonyesha na kuwaruhusu kinamama kuwa na muda wakunyonyesha watoto wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Henrietta Fore, alisema unyonyeshaji ni msingi wa kujitolea.

“Kuanza kunyonyesha ndani ya saa ya kwanza ya kuzaliwa, ikifuatiwa na unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa miezi sita na kuendelea kunyonyesha hadi miaka miwili au zaidi ni ulinzi dhidi ya aina zote za utapiamlo wa watoto, pamoja na kuondoa kunenepa kupita kiasi,” alisema Fore.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya Wiki ya Unyonyeshaji ni 'Kinga Unyonyeshaji: Jukumu la Pamoja'.

Katika hatua nyingine UNICEF imetoa mwongozo wa unyonyeshaji katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa corona.

Mwongozo huo umeeleza mambo kadhaa ikiwamo mama anayenyonyesha anaruhusiwa kupata chanjo ya corona na iwapo anahisi kuumwa anaruhusiwa kuendelea kumnyonyesha mtoto kwa kutumia kikombe kisafi, anatakiwa kuzingatia miongozo yote ya usafi ikiwamo kunawa mikono.

Mwongozo huo umetanabaisha hakuna taarifa yoyote iliyoonyesha mtoto ameambukizwa ugonjwa wa virusi vya corona kutoka kwa mama anayenyonyesha, hivyo hata mama akibainika amepata maambukizi anatakiwa kuendelea kunyonyesha mtoto.

Chanzo: ippmedia.com