Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

WHO: Kifua kikuu kinaua watu 70 kila siku Tanzania

48243 Pic+WHO

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu 70 wanafariki kila siku sawa na wastani wa watu watatu kila saa, kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa leo Machi 23 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu (TB) Duniani ambayo huadhimishwa Machi 24 kila mwaka.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa TB na inakadiriwa kuwa watu 154,000 huugua ugonjwa huo kila mwaka nchini.

Hata hivyo Waziri Ummy alisema kwamba hizo ni takwimu za WHO na kwamba kwa sasa Serikali iko katika mkakati wa kukusanya takwimu zake yenyewe katika vituo vya afya na hospitali nchi nzima.

“Takwimu za WHO zinaonyesha kwamba takribani watu 154,000 wanaugua kila mwaka, ni sawa na wagonjwa 269 katika kila Watanzania 100,000 ambapo makadirio yanaonyesha nchi inapaswa kufikia idadi hiyo ya watu na kuwaingiza katika matibabu, lakini vilevile husababisha vifo takribani 70 kwa siku sawa na vifo vitatu kwa saa moja,” amesema Ummy.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema tangu awamu ya tano ianze, wamefanikiwa kugundua  idadi ya wagonjwa wapya wa TB kutoka 62,180 hadi kufikia 75,845 mwaka 2018 na kuvuka malengo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kufikia wagonjwa 74,200.

“Mgonjwa ambaye hajaanza matibabu anaweza kuambukiza kati ya watu 10 hadi 20 kwa mwaka, katika hili tunalo jukumu kuhakikisha kwamba tunawafikia wote wanaougua na kuzuia maambukizo mapya,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz