Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vituo vya huduma za tiba na uokoaji kuanzishwa barabarani

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali kupitia wizara ya afya, inatarajia kuanzisha vituo saba vitakavyotoa huduma za tiba za uokoaji na usafirishaji wa majeruhi wa ajali vinavyojengwa kutoka barabara ya Dar es Salaam hadi Iringa.

Vituo hivyo vitajengwa Kimara, Tumbi, Chalinze, Mikese, Morogoro, Mikumi na Ruaha Mbuyuni, kupitia mradi wa EMS.

Akizungumza leo Jumanne Novemba 13, 2018 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watoa huduma hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya amesema mradi huo wa majaribio umeanzia barabara hiyo kwa kuwa ndiyo inayoongoza kwa ajali.

“Mkakati huu ulianza mwaka 2016, tumeanzisha mradi maalum utakaoshughulikia uokoaji na usafirishaji wa majeruhi wa ajali kupitia barabara hiyo kwa sababu baada ya utafiti tukagundua barabara inayoongoza ni ile ya kutoka Dar hadi mpaka wa Zambia,” amesema .

Amesema Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imetenga kiasi cha Sh8 bilioni kwa ajili ya uwekezaji na Sh2.5 bilioni kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za wataalamu.

Amesema kufanikiwa kwa mradi huo kutaleta chachu na kuhamasisha miradi hiyo kuendelea kote nchini.

Hata hivyo, amesema kuna haja kwa Mamlaka ya barabara Tanzania (Tanroads) kuangalia upya kufanyia kazi ufundi wa usanifu wa barabara ili kuepusha ajali.

“Serikali tutawekeza kwenye vifaa kusaidia wagonjwa kwa haraka zaidi, kuwepo kwa vifaa hivi havitakaa kusubiri ajali pekee, hivi vitakiwepo kwa ajili yakukidhi dharura mbalimbali,” amesema.

Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Maafa na Dharura, Dk Elias Kwessi amesema mradi huo shirikishi wa huduma za dharura na uokoaji unaanza kwa majaribio kupitia mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Iringa kupitia Kimara, Tumbi, Mikese, Morogoro, Mikumi na Ruaha Mbuyuni.

Amesema mradi huo unashirikisha wadau mbalimbali na unasimamiwa na wizara kupitia Muhas huku ikishirikisha Jeshi la polisi, Zimamoto na uokoaji, Jeshi la Wananchi, Tanroads, Redcross, baraza la usalama barabarani.

“Tumeagiza gari ya wagonjwa moja kwa moja kutoka kiwandani ambazo zina kila kitu ndani ya gari, tumeagiza magari maalum kwa ajili ya kukatia magari na ukarabati wa vituo umeanza,” amesema Dk Kwesi.

Makamu wa Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS,  Profesa Aporinaly Kamuhabwa amesema chuo kimeandaa mitalaa mitano kwa watahiniwa kwa kuhudumia magonjwa ya hospitali ya wiki sita kwa wataalamu wa afya.

“Mafunzo ya wasaidizi ya wiki nne kwa wasaidizi wa wataalamu wa afya, mfumo wa kupokea simu za wagonjwa wa dharura, mafunzo ya watoa huduma za dharura katika jamii na wakufunzi wa watoa huduma ambao wamekidhi vigezo vya kuwa wakufunzi,” amesema.

Profesa Kamuhabwa amesema awamu ya kwanza wataalamu 25 watapata mafunzo na ifikapo Februari  200 watakuwa wameshapata mafunzo hayo.



Chanzo: mwananchi.co.tz