Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vituo vya afya sasa kukaguliwa

Image1024x768 Vituo vya afya sasa kukaguliwa

Thu, 21 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuanza kukagua ubora wa vituo vya afya na kuvishauri vile ambavyo havitakidhi mahitaji yanayoruhusu kutoa huduma hizo.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi katika mkutano wa viongozi wa vyama vya kitaaluma vya Afya uliofanyika jijini Dar es salaam.

“Kuanzia wiki ijayo tutaanza na hospitali ya Taifa Muhimbili tunataka kukagua ubora wa huduma, kwa kushirikiana na menejimenti na vyama vya kitaaluma ili tuweze kuboresha maeneo ambayo yanalalamikiwa na wananchi,” amesema.

Prof. Makubi amesema watumishi wa sekta ya afya wanatakiwa kuboresha utoaji wa huduma za afya kama ilivyo ajenda ya kwanza kwenye sekta ya afya mwaka huu.

“Tunachotaka kuona sasa hivi ni ubora gani mwananchi amepata anapoenda kwenye kituo kwa kupokelewa kwa lugha nzuri na wahudumu, kusikilizwa na daktari kwa lugha nzuri, kupata vipimo kwa usahihi, kupata dawa ambazo ameandikiwa na daktari,” alisema Profesa Makubi.

Vile vile Prof. Makubi amewataka watumishi wa sekta ya afya kuwahudumia wagonjwa  kwa muda mfupi pindi wanapohitaji huduma na kuwahudumia kwa ubora wa hali ya juu.

“Tuachane na tabia ya mwananchi anaenda kwenye kituo anakaa kuanzia saa mbili mpaka saa nane bila kupata huduma, tuanze kupunguza muda wa kuwahudumia wananchi pia tuwahudumie kwa ubora,”

Aidha,Prof. Makubi amevitaka vyuo vya afya nchini kutoa elimu bora ili kuweza kupata wataalamu wenye viwango vya kuweza kulinda maisha ya wananchi na wizara itashirikiana na wizara ya elimu kurekebisha changamoto hizo ilikuweza kupata wataalamu wenye viwango.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt . Aifello Sichalwe ametoa wito kwa wasimamiaji wa huduma kuhakikisha wanafuata ubora wa huduma kwa wananchi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuzuilika ikiwemo vifo.

Kwa upande mwingine, Dkt. Sichalwe ametoa wito kwa Wanataaluma kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa (survaillence) ili kutambua mapema magonjwa, ikiwemo magonjwa ya mlipuko na kuweka mikakati mizuri ya namna bora ya kupambana dhidi ya magonjwa hayo kwa kushirikiana na Serikali.

Kwa upande wake msajili wa Baraza la famasia Bi. Elizabeth Shekalaghe ametoa wito kwa wanataaluma wa afya wote nchini kuhakikisha wanazingatia sheria kanuni na miongozo katika utendaji kazi wao.

“Faini kwa wanataaluma wanao fanya makosa zipo, kwa hiyo nitoe wito kwa wanataaluma wote nchini kufuata sheria kanuni na miongozo wakati wa kutoa huduma.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live