Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vituo vya afya 121 kujengwa

330ea60a2c8da7fd460ad6e390d5a18c Vituo vya afya 121 kujengwa

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VITUO vya afya 121 vinatarajiwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa kutumia fedha kutoka serikali kuu na mapato ya ndani ya halmashauri mbalimbali.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakatwe (CCM) aliyetaka kufahamu ni lini serikali itaongeza vituo vya afya katika jimbo hilo lenye kata 24 lakini lina vituo vya afya viwili pekee.

Dk Dugange alisema nchi nzima kuna kata 3,900, hivyo serikali itajenga vituo vya afya kwa awamu kwani haitaweza kujenga kwa wakati mmoja, hivyo mwaka ujao wa fedha vitajengwa vituo 121 katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Nkasi Kusini, Vicent Mbogo (CCM) alisema jimbo hilo lina kata 11 na kituo cha afya kimoja pekee na kutaka kujua kama serikali ina mpango wa kuongeza vituo vya afya hasa katika tarafa za Chala, Kate, Myula, Sintali na Ninde.

Alisema katika kuboresha huduma za afya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, serikali imejenga na kukarabati vituo vya afya vya Nkomolo na Kirando kwa gharama ya Sh milioni 900.

“Pia serikali imetoa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na katika mwaka wa fedha 2020/21 imetenga Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu na Sh milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali hiyo,” alisema.

Dugange alisema pia serikali imetenga Sh milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matatu ya zahanati katika halmashauri ya wilaya ya Nkasi.

Aidha, alisema halmashauri ya wilaya hiyo inakamilisha utaratibu wa kuingia makubaliano ya utoaji wa huduma na Kituo cha Afya Mzimwa kinachomilikiwa na taasisi ya kidini ya Kanisa Katoliki Abei kwa ajili ya wananchi kupata huduma za afya ikiwamo za upasuaji wa dharula, ambapo wananchi wa tarafa za Myula na Sintali ni miongoni mwa watakaonufaika.

Alisema halmashauri hiyo imetenga eneo katika tarafa ya Chala kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya kupitia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri mwaka wa fedha 2021/22.

Chanzo: www.habarileo.co.tz