Dar es Salaam. Mkoa wa Kigoma umenufaika na mradi wa Afya ya Mama na Mtoto mradi uliofanikisha kuboresha vituo vya afya 100.
Mradi huo ambao umedhaminiwa na Meya wa Marekani, Michael Bloomberg kupitia Taasisi ya Bloomberg Phalanthropies ya New York City kwa kushirikiana na Taasisi za Thamini Uhai, Engender Health na H&B Agerup, ulianzishwa mwaka 2006 katika mikoa ya Kigoma, Pwani na Morogoro.
Dk Godson Maro ambaye ni mratibu wa Afya ya mama na mtoto kutoka Taasisi ya Bloomberg, ameliambia Mwananchi leo Jumapili Juni 23,2019 kuwa awali Mkoa wa Kigoma ulikuwa na changamoto nyingi za afya ya mama na mtoto hasa ya wazazi wengi kujifungulia nyumbani.
“Kupitia mradi huu sasa, zaidi ya watoto 210,000 wamezaliwa kwenye vituo vya afya vilivyoboreshwa,” amesema Maro.
Amesema Serikali ya Tanzania ilikuwa na maono ya kupeleka huduma za kuokoa maisha ya mjamzito maeneo ya pembezoni kuliko na changamoto nyingi na kwa Kigoma imefanikiwa.
Maro amesema mkoani Kigoma mradi huo umeboresha kwenye vituo vya afya 100 ambavyo ni hospitali tatu, vituo vya afya 13 na zahanati 82 kwa kusaidia upatikanaji wa dawa muhimu, vifaa tiba na vitendea kazi.
Pia Soma
- Hatimaye watoto pacha walipotea wapatikana, walikuwa wakifuata ng’ombe
- Wanafunzi wa miaka 13 na 16 wadakwa wakiishi unyumba
- VIDEO: Michango ya harusi ilivyotumika kumzika bi harusi mtarajiwa
Amesema licha ya mradi huo kufikia tamati, lakini umeacha huduma katika mkoa huo zikiendelea ikiwamo matumizi ya uzazi wa mpango ambao umetoka asilimia 15.6 mwaka 2014 na kufikia asilimia 21 mwaka jana.